RIPOTI MAALUM-Biashara ya kutisha Dar,ombaomba watumika

Muktasari:

Lakini kwa sababu za kijamii, ni muhimu kuangalia kwa kina mfumo mzima wa watu wanaoomba mitaani, hasa wenye ulemavu unaowafanya wasiweze kabisa kujishughulisha na kazi za uzalishaji.

Dar es Salaam. Kusaidia maskini ni kutoa sadaka na kwa wengine ni ibada. Hivyo si rahisi kwa mtu kufuatilia alichokitoa kinatumikaje au kinakwenda wapi kwa kuwa jukumu lake lilikuwa ni kutoa sadaka au kufanya ibada.

Lakini kwa sababu za kijamii, ni muhimu kuangalia kwa kina mfumo mzima wa watu wanaoomba mitaani, hasa wenye ulemavu unaowafanya wasiweze kabisa kujishughulisha na kazi za uzalishaji.

Umeshawahi kujiuliuliza wale ombaomba walemavu wanaotumia viti vya magurudumu wana uhusiano gani na vijana wanaowasukuma? Je, ni ndugu au vijana tu walioamua kuwasaidia?

Wengi hujiuliza, hawa wanaowasukuma ombaomba walemavu ni vijana wenye afya njema na nguvu. Kwa nini basi wasijihusishe na shughuli za uzalishaji au biashara ili wawasaidie hao ndugu zao badala ya kufanya kazi nzito ya kuwasukuma kutwa nzima na kutembea sehemu kubwa?

Umewahi kujiuliza kuwa hawa vijana wanawapa fedha hao ombaomba walemavu kwa kadri wanavyopata au wanawadhulumu? Umewahi kujiuliza hawa walemavu wanaoomba wanalala wapi? Mbona hawaonekani kwenye makazi ya kawaida tunayoishi?

Umewahi kujiuliza wazazi wa hawa walemavu wanaoomba, wapo wapi? Je, ni wao wanaowaruhusu hawa vijana kuwachukua asubuhi na kuwarudisha nyumbani jioni? Na kama hawawaruhusu, hawa walemavu wanatokea wapi na kuna makubaliano gani kati ya wazazi na hao vijana?

Mwananchi linaweza kukuthibitishia kuwa hao wenye ulemavu wanaozungushwa mitaani kuombaomba ni mpango mzito wa wajanja wanaojinufaisha kwa kutumia udhaifu wao.

Mwandishi wetu, Jackline Masinde ameongea na walemavu hao, vijana wanaowasukuma, ameishi nao na kufuatilia hadi kijiji walichotoka baadhi yao na kuzungumza na wazazi.

Masinde anasimulia habari hii ya uchunguzi kuhusu maisha ya walemavu wanaoomba na mradi wa wajanja kujinuisha uliojificha nyuma yao.

Kwa mtu usiyependa kudadisidadisi, unaweza kuiona nyumba iliyo na bango lililoandikwa Sir Herman (si jina halisi) iliyopo Manzese kuwa ni nyumba ya kawaida ya kulala wageni.

Ni maeneo ya kituo cha Bakhresa, Manzese kuliko na nyumba hii ambayo si rahisi kwa wageni wa kawaida kwenda kuishi kutokana na hali ya usafi kuwa si nzuri.

Ndani ya nyumbani hii wanaishi walemavu wanaofanya shughuli za kuombaomba mitaani, wakitumia viti vyenye magurudumu na kusukumwa na vijana wenye nguvu.

Katika nyumba hii, ninamkuta mmoja wa walemavu hao ambaye baadaye nagundua kuwa jina lake ni Ndebhile ambaye ana umri wa miaka takriban 12. Ni mlemavu wa miguu na hawezi kutumia vizuri mikono yake.

Wakati nilipofika, nilikuta anakula chakula akiwa karibu na choo ambacho kinaonekana kimeziba na hivyo uchafu kupanda juu.

Maji machafu yaliyochuruzika kutoka chooni yanapita karibu na sehemu alipoketi Ndebhile na ilipo sahani yake ya wali na maharage.

Lakini Ndebhile akiwa amevishwa nguo mithili ya nepi, anakula chakula bila ya wasiwasi.

Kutokana na ulemavu wake, analazimika kushika chini kwa kutumia mikono yake iliyotapakaa wali na maharage na ambayo anaitumia kuchota chakula hicho na kukipeleka mdomoni.

Hili ni moja kati ya mambo niliyoshuhudia wakati nilipoenda kufuatilia maisha ya watu wenye ulemavu wanaozungushwa mitaani kuomba wakiwa na vijana wenye nguvu.

Siku nilipoanza kuwafuatilia ilibidi nijivishe kama wanavyovaa ombaomba wengi maana ukienda kwa Waroma, fanya kama wafanyavyo.

Nilivaa nguo zilizochakaa ili nifanane na ombaomba kabla ya kuondoka nyumbani saa 4:00 asubuhi kuelekea kituo cha daladala cha Gerezani, ambako walemavu wanaoomba, huweka kambi hapo kutokana na eneo hilo la Kamata kuwa lina watu wengi wanaoshuka kutoka kwenye mabasi yanayotoka karibu kila kona ya jiji.

Eneo hili lina msongamano mkubwa wa watu na shughuli ni nyingi.

Kwa watu hawa wanaoomba, abiria hao ni matajiri wao.

Ombaomba walikuwa wamekaa nje ya lango la kituo cha daladala na ndani ya kituo.

Ombaombao ambao ni walemavu pia hukaa maeneo hayo, lakini kwa mtindo wa kipekee. Huwa kwenye mstari kama vile wamepangwa. Viti vyao vya magurudumu hufungwa vikombe maalumu ili kwa wale wanaoguswa na hali zao, waweze kutumbukiza fedha.

Hawa pia wanaenda na mabadiliko ya kiteknolojia kwa kuwa wana vipaza sauti vya kielektroniki vilivyorekodiwa sauti ya kuomba msaada, mithili ya wauza mitumba au wafanyabiashara ndogondogo wa maeneo ya Kariakoo.

Moja ya vifaa hivyo vya kielektroniki kilikuwa kikitoa sauti isemayo “watu wa Mungu, mimi ni mlemavu wa macho, naomba msaada wenu. Kutoa ni moyo, mtabarikiwa sana.” Hiki ni kipaza sauti cha mwanamke mlemavu aliyekuwa na watoto wawili, mmoja akiwa amembeba mgongoni.

Hakuna shaka kwamba sauti hiyo ilitosha kushawishi baadhi ya watu kutumbukiza kwenye kikombe chake chochote walichokuwa nacho, hasa wanafunzi na wanawake.

“Ukisaidia watu wasiojiweza utabarikiwa. Unaweza kushangaa uko ndani ya chumba cha mtihani majibu yanamiminika tu,” alisema mmoja wa wanafunzi waliotoa msaada kwa mama huyo wakati akizungumza na mwenzake na baadaye wote wakacheka.

Huyu si peke yake aliyekuwa na kipaza sauti. Kipaza sauti cha mlemavu mwingine kijana ambaye muda wote alikuwa amefumba macho, kilikuwa kikisema: “Ee Mungu wape moyo wa huruma wapate kunisaidia.”

Waombaji hao wanaonekana kuwa wasiozingatia usafi na ambao muonekano wao huvuta hisia za huruma. Baadhi hushindwa kuzuia mate kuchuruzika kutoka mdomoni na wanalala sehemu yenye vumbi.

Kwa siku, eneo hili huwa na ombaomba wapatao 15, kati yao saba wana ulemavu wa macho, wanne ni wenye vichwa vikubwa na waliobaki ni walemavu wa miguu.

Ni watu wanaostahimili mazingira yao ya kufanyia kazi. Hata jua linapokuwa kali, humudu kukaa muda mrefu kana kwamba haliwasumbui.

Pamoja na hali zao duni, kuna watu wanaowaangalia na kuwajali kwa chakula.

Kila inapofika mchana kuanzia saa 7:00 kuna kijana anayeonekana kuwa na umri wa miaka kama 35, huenda kwa yule mama mwenye watoto watatu na kumpa chakula.

Lakini mama huyo na wanawe hutumia eneo hilohilo lenye vumbi linalotimuliwa na wapita njia na lisilo na faragha, kula chakula chake cha mchana. Kijana huyo huondoka baada ya mlemavu huyo kumaliza kula.

Na si mama huyo pekee aliye na mtu anayeonekana kuwa ni msamaria. Kilichoonekana kwa mama huyo ndicho kilivyo kwa walemavu wengine.

Walemavu hawa huwa na vijana wa kiume wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 25. Muda wote vijana hawa wanakuwa wamekaa pembeni wakitazama tu.

Vijana hao hujitokeza pale wanapoona kuna mtu anazungumza na ombaomba au ameona kitu kisicho cha kawaida. Lakini kazi yake inakuwa ni kusikiliza kinachoongelewa kati ya ombaomba na huyo mtu.

Vijana wanaowasukuma walemavu, pia hufanya kazi ya kupiga debe au biashara ndogondogo.

Wengine huzungukazunguka eneo hilo au kujilaza kivulini, lakini hutumia muda mwingi kuwaangalia ombaomba wao. Mawasiliano baina ya vijana hao ni ishara.

Mfano anaweza kuja kijana mmoja akasimama kwa ombaomba mmoja na kujifanya anapiga simu, baada ya dakika chache hutokea kijana mwingine. Baadaye vijana hao hukusanyika wengi na kuzungumza jambo kwa sekunde chache kabla ya kutawanyika.

Dakika chache baadaye, kila mmoja huenda kwa wakati wake kumchukua ombaomba wake.

Baada ya kuwafuatilia, niligundua kuwa vijana hao huenda na ombaomba hao hadi eneo ambalo halina watu wengi na kuchukua fedha zilizo kwenye kikombe kwa ajili ya kuzihifadhi. Baadaye wanajizungusha kwa muda, kisha hurudi kituoni, na kitendo hicho hufanywa na vijana wengine wote.

Wanajua kuigiza

Ni hulka ya binadamu kuingiwa na huruma anapoona watu kama hao wakiomba na wengi huamini kuwa wanapata thawabu kwa kuwapa chochote walichonacho. Lakini, baadhi ya ombaomba hao hufanya maigizo.

Wanajua kujiweka katika hali ambayo huwafanya waonekane wana dhiki kiasi cha kuonewa huruma.

Haya ndiyo ninayoyashuhudia baada ya kuamua kuzungumza na vijana wanaowasukuma walemavu hawa na walemavu wenyewe ili kujua ukweli kuhusu maisha yao.

Shadrack anayedai kuwa ni mwenyeji wa Mkoa wa Shinyanga, ndiye mwenye mtoto aliye na kichwa kikubwa niliyemkuta nje ya kituo cha mwendokasi cha Kamata jirani kabisa na lango kuu.

Mbali na kuwa na kichwa kikubwa, mlemavu huyu anatokwa na mate mdomoni yanayovutia nzi ambao wanapishana puani na mdomoni kwake.

Najaribu kuzungumza naye na anaishia kucheka na kutamka neno “dada”.

Lakini mama aliyekuwa jirani ananiuliza nina shida gani na baadaye anaonyesha ishara ya kumtaka mtu anayeshughulika na mlemavu huyo ajongee.

“Unasemaje dada?” anauliza kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Shadrack na baada ya kumuambia namtaka mtu aliye na mtoto huyo ananijibu kuwa ni yeye.


ITAENDELEA KESHO