Bibi Cheka huyu hapa kivingine

Bibi Cheka

Muktasari:

Nyumba yake ya vyumba vitatu iliyozungushiwa uzio wa mabati inatosha kuonyesha maisha halisi anayoishi Bibi Cheka.

Ni takribani kilometa 39 kutoka Tabata zilizopo ofisi za Mwananchi, ambapo mwandishi wa makala hii anafunga safari kwenda kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya Cheka Hija maarufu ’Bibi Cheka’.

Nyumba yake ya vyumba vitatu iliyozungushiwa uzio wa mabati inatosha kuonyesha maisha halisi anayoishi Bibi Cheka.

Nilipobisha hodi nilikutana na mama ambaye anaonekana bado ni mdogo kiumri akiwa anawanywesha watoto wake wawili wadogo uji.

Hiyo ilikuwa majira ya saa saba wakati wakinywa uji huo, muda ambao kwa kawaida ni wa kula chakula cha mchana.

Anatoka na ninapojitambulisha kwake na kisha kumwambia nimekwenda kwa ajili ya kumuona Bibi Cheka, ananijulisha kwamba hayupo, ameenda kwenye shughuli ya hitma ambayo ni karibu na hapo nyumbani na kunitaka nimsubiri akamuite.

Nilipomuuliza yeye ni nani kwake, alinijibu kwamba ni mkwewe.

Hatimaye Bibi Cheka anakuja akiwa amevaa dera lake la rangi ya njano lililochanganyika maua ya rangi ya dhambarau, huku chini akiwa kavaa kandambili.

Kwa ukarimu bibi huyu anachukua mkeka na kunikaribisha chumbani kwake kwa kuutandika chini na hapo ndipo tunapoanza mahojiano yetu kujua nini kilichomfanya awe kimya muda wote huo na maisha anayoishi kwa sasa.

Kwa msiomkumbuka

Mwaka 2012 wimbo wa ‘Ni Wewe’ ndio uliomtambulisha vyema bibi huyu aliyekuwa akisimamiwa na uongozi kundi la Wanaume TMK Family na kushika nafasi ya juu katika chati ya muziki katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni.

Msanii huyo ambaye ndiye mwenye umri mkubwa wa wasanii wanaofanya muziki wa aina hiyo nchini, alijikuta akiangukia katika kundi hilo baada ya kuibuliwa maeneo ya Bunju kwenye sherehe ya makundi ya vijana maarufu kama ’Camp’.

Akiwa katika kutumbuiza mmoja wa wasanii kutoka kundi la TMK, Mh Temba alitambulishwa na vijana wanaomjua bibi huyo kwake na kumweleza kwa anajua kuimba na kuomba asaidiwe.

Naye Temba bila hiana alimpeleka kwa bosi wao Said Fella.

Kwa mujibu wa Fella alikubali kumchukua baada ya bibi huyo kumueleza namna alivyo na matatizo ya kimaisha ikiwemo kufiwa na watoto wake nane kati ya kumi na wawili ambao ni Adam(30) na Kombo(20) hawana msaada wa hivyo kwake kutokana na wao kuwa na maisha magumu na bado wana familia zao zinawategemea.

Alikuwa wapi na sasa anafanya nini

Katika maelezo yake Bibi Cheka anasema ni takribani miaka mitatu sasa amesimama kazi ya muziki kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuumwa.

Anasema alikuwa akisumbuliwa na miguu hadi ilifika mahali akawa hawezi kusimama peke yake bila msaada wa kushikwa na mtu.

Anaeleza kuwa anashukuru kwa sasa anaendelea vizuri na kudai yupo tayari kurudi kwenye kazi ya muziki kama atapata meneja wa kumsimamia au mdhamini wa kumuingiza studio. Bibi huyo wa miaka 60 sasa, anasema kwa sasa hana kazi ya kufanya na anaishi kutokana na kipato kidogo cha watoto wake wawili ambao wamekuwa wakijishughulisha na kutengeneza vifaa vya umeme.

Kuhusu muziki, anasema bado anahitaji kufanya kazi hiyo na kuongeza kuwa mpaka sasa ana nyimbo tatu alizozitunga na anachosubiri ni kuingia studio kuzirekodi ambazo anaamini zitafanya vizuri kama atapata promo nzuri.

Kusimama kwake tena kimuziki anasema kutamwezesha kuendesha maisha yake kwa kuwa sasa hivi kila kitu anawategemea watoto wake hao wawili ambao nao wana familia zao, huku yeye akiwa na mzigo wa wajukuu wengine ambao wazazi wao walifariki.

Kuondoka kwake TMK

Anasema hakumbuki ilikuwa mwezi gani lakini ni kama miaka minne imepita sasa tangu alipoitwa na mkubwa Fella na kuambiwa kuwa hawawezi kuendelea naye tena na kumtaka akajitegemee kuendeleza kipaji chake.

Katika kuagana naye huko, anasema walichompa ni matofali 400, saruji mifuko 50 na fedha Sh150,000 kwa ajili ya kumlipa fundi wa kumjengea nyumba kama kifuta jasho.

Bibi huyu anasema TMK walimfanyia hayo wakati hayakuwa makubaliano naye, kwani awali ilikuwa wameafikiana kwamba wangemjengea nyumba ya kisasa.

“Lakini ndio kama hivyo waliamua kunipa vitu hivyo na mimi sikuwa na namna ya kwenda kulalamika mahali ikabidi nikubaliane nao tu japokuwa nyumba iliishia kwenye madirisha na palipobakia ilibidi niuze kipande changu cha ardhi niweze kuweka bati na madirisha niingie.

“Nilifanya hivyo kwa kuwa nyumba niliyokuwa naishi ni ya udongo ilibomoka mwaka juzi katika msimu wa mvua na kwa kipindi chote hicho tuliegesha mabati juu ili tupate pakujisitiri mimi, watoto wangu na wajukuu zangu watano.

Pia, anabainisha kwamba katika maisha yake yote akiwa anafanya kazi na TMK, alikuwa akilipwa Sh100,000 na wakati mwingine Sh200,000 kila wanapoenda kwenye shoo, huku hela kubwa anayokumbuka kupewa kwa mara moja ilikuwa Sh300,000.

Mkubwa Fella afunguka

Kwa upande wake Mkubwa Fella anasema bibi huyo wakati anaenda TMK alitaka asaidiwe ili aweze kuendesha maisha yake na ndipo alipoamua kumuingiza studio ilimradi na yeye jamii iweze kumtambua.

“Kama mlivyomuona sio kwamba ana kipaji cha hivyo lakini kama binadamu niliona kwa kuwa ana shida basi nimtengeneze kwa hicho kipaji alichodhani anacho ili naye aweze kuingiza mkono kinywani.

“Niwaambie tu kwamba haikuwa kazi ndogo kumtengeneza hadi mkaona ule wimbo wa ‘Ni Wewe’ alioimba na Temba umetoka, japo tunashukuru watu walimpokea naye akawa anapata sh. Mbili tatu tunapoongozana naye kwenye shoo.

Kuhusu suala la kuingia naye mkataba wa kumjengea nyumba ya kisasa, hilo halina ukweli wowote na kama ana uhakika na hilo analoliongea mwambieni awaonyeshe mkataba tulioandikishana.

Anasema: “Wakati mwingine unajitahidi kuwa mwema kwa watu lakini mwisho wa siku wanakuja kukubebesha lawama zisizostahili”.

Wakati kwa upande wa kuondoka kwake TMK, anasema chanzo kilikuwa Bibi Cheka alipata watu wakamdanganya kuwa wangemsimamia kimuziki lakini mwisho wa siku wakamuachia barabarani.

Hata hivyo, anasema waliona sio vyema kumuacha aondoke hivihivi ndio wakampa hayo matofali, saruji na kumlipia hela ya fundi ya kujengea nyumba ambayo ataweza kujihifadhi kutoka ile ya udongo.