Bibi aliyejichongea jeneza afariki dunia

Sh 70,000: Fedha zilizotumika kununulia jeneza la kumzikia.

Muktasari:

  • Waliovunja jeneza lake na kuahidi kumtengenezea jingine walichelewa kupata taarifa za msiba

  • 76: Umri aliokuwa nao hadi anafariki dunia.

Songea. Mkazi wa Kijiji cha Lindusi Peramiho mkoani Ruvuma aliyejichongea jeneza, Scholastica Mhagama amefariki dunia  kwa ugonjwa wa pumu.

Mapema mwaka huu wakati alipohojiwa na gazeti hili, bibi huyo alitaja sababu za kujichongea jeneza kabla ya kifo kuwa, ni kuhofia kuzikwa kama mnyama baada ya kuwa na ugomvi wa mara kwa mara na kaka zake.

Kaka yake mkubwa aliyekuwa akimhudumia kabla ya kufariki dunia, Felix Mhagama (82) alisema dada yake alikufa Jumanne ya wiki iliyopita kwa ugonjwa huo.

Mhagama alisema licha ya kipindi cha uhai wa dada yao, kugombana mara kwa mara walikuwa wakipatana na kumaliza tofauti zao.

“Ingawa mdogo wangu alikuwa na upungufu niliendelea kuzungumza naye na kumhudumia, kwani hakuwa na uwezo wa fedha na alinitegemea kwa kila kitu,” alisema. Alisema alikuwa akiumia kuona dada yake akiishi na jeneza hilo na kwamba, kuna wakati alimuuliza sababu za kufanya hivyo, alimjibu kuwa ni kutokana na kutokuelewana kwao.

Alibainisha kuwa kabla ya kifo chake, kuna watu walikwenda nyumbani kwake na kuvunja jeneza hilo na kuahidi kumtengenezea jingine.

Kuhusu chanzo cha ugomvi wa Scholastica na kaka zake, jirani yao, Cassian Kazimoto alisema  alikata tamaa ya kuishi kutokana na maradhi hayo ya pumu yaliyokuwa yakimsumbua na ulemavu baada ya kukatwa mguu.

Alisema  Scholastica alikuwa akiona kama anaonewa na kaka zake kutokana na ugomvi wao.