Malaria yatikisa Afrika

Muktasari:

Vifo vitokanavyo na malaria vimekuwa vikipungua tangu mwaka 2000, lakini vilianza kuongezeka tena mwaka 2016 kutokana na kudorora kwa juhudi za kupambana na maradhi hayo yanayoenezwa na mbu.

London, Uingereza. Bilionea raia wa Marekani,  Bill Gates   amesema maambukizo ya ugonjwa wa malaria yameongezeka na yatazidi kuenea, ikiwa viongozi  hawatakuwa na jitihada za kuutokomeza.

Vifo vitokanavyo na malaria vimekuwa vikipungua tangu mwaka 2000, lakini vilianza kuongezeka tena mwaka 2016 kutokana na kudorora kwa juhudi za kupambana na maradhi hayo yanayoenezwa na mbu.

Bill Gates alikuwa akizungumza katika mkutano wa kimataifa kuhusu malaria unaofanyika mjini London, Uingereza.

Takwimu zinaonyesha kuwa malaria iliwaua watu 445,000 mwaka 2016 wengi wao wakiwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito.

Kadhalika, mwaka huo kulikuwa na maambukizo ya ugonjwa huo milioni 216 huku asilimia 90 yakiwa kutoka barani Afrika.