Saturday, March 18, 2017

Bila kusameheana CUF iko hatarini kufutwa na msajili

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) akiwaongoza viongozi wa chama hicho kuingia makao makuu kuhudhuria moja ya vikao vya juu Aprili 2015. Anayefuata ni aliyekuwa makamu wake (Zanzibar), Juma Duni Haji; Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad. Picha na Maktaba 

By Masoud Sanani

Chama cha Wananchi (CUF) ni moja ya vyama vikongwe vya siasa nchini ambavyo vimekuwa na maendeleo tangu kuanza kwa mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini mwaka 1992.

Miaka ya nyuma, CUF iliwahi kuwa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania kabla ya kuondolewa hivi karibuni na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kwa sasa ndicho kinaongoza upinzani.

Mbali na hilo, CUF ndicho chama cha siasa chenye nguvu zaidi kwa upande wa Zanzibar, katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Katika chaguzi mbalimbali zilizopita, CUF imekuwa inashinda majimbo yote ya kisiwa cha Pemba na baadhi ya majimbo ya Unguja na kukiacha Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kinachotawala kikipata baadhi ya majimbo ya kisiwa cha Unguja pekee.

Hata hivyo, CUF hivi sasa haina uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar na mabaraza ya miji, baada ya CCM kushinda viti vyote vya uwakilishi na madiwani kutokana na chama hicho cha upinzani kukataa kushiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar baada ya matokeo ya ule wa Oktoba 25, 2015 kufutwa.

Mgogoro wakomaa

Kwa sasa CUF ipo katika mgogoro mkubwa uliosababishwa na Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alijiuzulu nafasi hiyo, lakini akaamua kurudi miezi 10 baadaye.

Kitendo hicho kimesababisha mgogoro ambao unazidi kufukuta na iwapo hakutakuwa na hatua za kuumaliza unaweza kukiyumbisha zaidi chama hicho.

Profesa Lipumba alijiuzulu miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 jambo ambalo lilikifanya chama hicho kuingia katika uchaguzi mkuu bila ya kuwa na mwenyekiti.

Hakuna mwenye uhakika kwamba uamuzi wa Lipumba wakati anajiuzulu ulikuwa na lengo gani, lakini kwa hisia za baadhi ya watu ni kwamba ulilenga kukifanya chama hicho kufanya vibaya katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, CUF ambayo ilishiriki katika uchaguzi huo ikiwa katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioundwa na vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na NLD ilifanya vizuri kuliko katika Uchaguzi Mkuu mwingine wowote ule.

Kwa upande wa Tanzania Bara, chama hicho badala ya kupata majimbo mawili au pungufu kama ilivyokuwa katika kila uchaguzi ilipata wabunge katika majimbo 10 na kwa mara ya kwanza ikaunda halmashauri za wilaya.

Kwa upande wa Zanzibar, kabla ya matokeo kufutwa CUF ilikuwa imeshinda viti 27 vya wawakilishi waliokabidhiwa vyeti vya ushindi sawa na CCM.

Hata mgombea wa Chadema na Ukawa kwenye urais wa Muungano, Edward lowassa akiungwa mkono na CUF yenye nguvu Zanzibar, alipata kura nyingi visiwani humo kuliko mgombea wa CCM.

CUF baada ya kufanya vizuri katika uchaguzi huo, Profesa Lipumba aliamua kurudi kwenye nafasi ya uenyekiti, jambo ambalo bila shaka yoyote ndilo limekiingiza chama hicho katika mgogoro mkubwa.

Inaelekea msomi huyo wa uchumi baada ya kugundua kuwa kujiuzulu kwake hakukuleta madhara yoyote, bali manufaa zaidi, akaamua kurudi katika nafasi hiyo na kuleta mgogoro.

CUF inapoteza mwelekeo

Katika mgogoro huu ambapo upande wa uongozi unaompinga mwanasiasa huyo kurudi madarakani ukiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ulimfukuza uanachama, lakini naye hakukubali na sasa ametengua vyeo vya wakurugenzi wa chama.

Akiungwa mkono na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ambaye alimtambua kuwa ni mwenyekiti halali wa chama hicho, Profesa Lipumba amekifanya chama hicho kuelekea kupoteza mwelekeo.

Hivi sasa CUF ambayo ina kesi mahakamani ipo katika wakati mgumu kwani ni vigumu katika mazingira waliyo nayo kuwashawishi wanachama wapya kujiunga au kupata wafuasi wapya hasa vijana.

Mazingira yanayoizunguka CUF ni vigumu kumshawishi mtu yeyote kujiunga nayo.

Hata hivyo, inatoa mwanya mkubwa kwa wanachama wa chama hicho kujiunga na vyama vingine.

Serikali inaweza kukifuta

Haieleweki dhamira ya Profesa Lipumba na mgogoro huu uliosababishwa na kurudi kwake kwenye uongozi, lakini kuna uwezekano kwa Serikali kukifuta chama hicho ambacho kilipata umaarufu mkubwa nchini.

Ni rahisi katika hali hiyo  mgogoro ukatumia mwanya huo Serikali ikakichukulia hatua na hata kukifuta kwa madai kwamba kinatahatarisha amani na utulivu nchini.

CUF itafute suluhu

Kuna haja kwa chama hicho kutafakari upya na kutafuta suluhu ya kuumaliza mgogoro huo kabla ya kuleta athari kubwa kwani Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 haupo mbali.

Inabidi kujipanga upya kuondokana na mgogoro huo ili iweze kufanya vizuri katika uchaguzi kwa upande wa Tanzania Bara ili isirejee kama miaka ya nyuma ya kupata wabunge wawili.

CUF ikiondokana na mgogoro huo itakuwa katika mazingira mazuri zaidi ya kufanya vizuri katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, hata kama usimamizi wa uchaguzi huo utakuwa na mizengwe kiasi gani.

Kwa upande wa Zanzibar, CUF ina nguvu kubwa ambayo kwa namna yoyote ile na kwa vyovyote haiwezi kuzuilika kushinda katika majimbo kadhaa ya Unguja na Pemba. Kwa hiyo uongozi unapaswa kutafakari na kutafuta njia ya kukiokoa chama chao na njia rahisi kuliko zote ni kusameheana na kuelewa kwamba yaliyopita si ndwele wagange yajayo.

Kutokana na mgogoro huo kuendelea kukimong’onyoa chama hicho hadi watu waliokuwa marafiki zamani kugeuka kuwa mahasimu, pengine dawa pekee ya kumaliza mgogoro huu ingepaswa kutoka nje ya chama baada ya jitihada za ndani kuonekana kugonga mwamba.

Hata hivyo, swali la kujiuliza ni nani atajitokeza kuifanya kazi hiyo ya kuwakabili mahasimu wawili, Profesa Lipumba na Maalim Seif na wafuasi wao ili  kuwasihi wakae pamoja na kumaliza sintofahamu zao kwa ajili ya mustakabali wa chama hicho?

Katika moja ya tahariri zake, gazeti hili liliwahi kupendekeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iingilie kati na kunusuru hali ya mambo, kwa kuwa msajili ndiye mdau na mhimili mkuu wa vyama vya siasa ambaye anaweza kujivika jukumu la usimamizi kwa sura ya ulezi na kuacha kubagua au  kuonekana kuwa na upande.

Mwandishi ni mwanahabari mwandamizi nchini na amefanya kazi Televisheni Zanzibar, magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Majira na Mwananchi. Anapatikana kwa baruapepe: sanani07@yahoo.com

-->