Takukuru yatekeleza amri ya Mahakama kumpeleka Sethi Muhimbili

Muktasari:

Swai ameeleza kutokana na hali hiyo, Sethi atarudishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuchukua majibu ya vipimo vyake wiki ijayo.

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetekeleza amri za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kumpeleka mshtakiwa katika  kesi ya uhujumu uchumi, Harbinder Sethi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai leo Ijumaa amemweleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa wametekeleza amri za Mahakama walizopewa kwa kumpeleka Sethi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kwamba kinachosubiriwa ni ripoti ya daktari.

Swai ameeleza kutokana na hali hiyo, Sethi atarudishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuchukua majibu ya vipimo vyake wiki ijayo.

Baada ya maelezo hayo wakili wa mshtakiwa, James Rugemalira, Respicius Didas ameeleza mahakamani hapo kuwa kuna suala la ucheleweshwaji wa upelelezi na kwamba washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Juni 19,mwaka 2017 na wapo ndani hadi sasa.

Wakili Didas ameeleza kuwa upande wa mashtaka unawaambia upelelezi bado haujakamilika, wateja wao wanaendelea kukaa ndani na kwamba kuna athari sana.

Akijibu hoja hiyo, Swai amesema kuwa uchunguzi wa kesi ya kughushi unachukua muda hivyo aliomba mawakili wa upande wa utetezi wajue upelelezi bado unaendelea na kwamba sheria ipo wazi katika masuala ya kughushi.

Hakimu Shaidi yeye  aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 27,2017 ambapo kesi hiyo itatajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Katika kesi hiyo, washtakiwa Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya  uhujumu uchumi kwa  kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kighushi, kutoa nyaraka za kughushi na  kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.

Pia wanakabiliwa na mashtaka matano ya kutakatisha fedha pamoja na  kusababisha hasara ya Sh 309.4 bilioni