Bilionea wa IPTL hajapata matibabu, Hakimu awa mkali

Muktasari:

  • Mahakama imeamua Sethi akatibiwe Muhimbili hivyo ihakikishwe kuwa amefikishwa huko

Dar es Salaam. Mshtakiwa Habinder Sethi ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa bado hajatibiwa.

Sethi amesema hayo mahakamani baada ya wakili wake kuomba aulizwe kama ametiwa na hakimu kumuujiza jambo lililomnyanyua Sethi ambaye alisema hajatibiwa

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema ni wazi amri ya Mahakama ni lazima zifuatwe.

"Hatuwezi kila siku kuongeza kitu kimoja, Mahakama nilisema apelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutibiwa kutokana na matatizo yaliyoelezwa mahakamani kuwa ana puto tumboni,"amesema Hakimu Shaidi.

Amesema Mahakama iliona ni busara apelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akatibiwe kwa sababu kuna wataalam.

"Matakwa yetu ni kuona mshtakiwa anakuwa na afya njema na anahudhuria kesi yake na kwa upande wa Serikali kesi hiyo inathibitika."

Hakimu Shaidi amesema mara ya mwisho upande wa mashtaka ulisema Sethi alikutana na mtaalam katika Hospitali ya Amana leo mtaalam kaenda Magereza kauli zinabadilika.

"Hainifurahishi kila siku kuongea hiki kitu hivyo apelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akatibiwe,"amesema Hakimu Shaidi.

Hakimu Shaidi alimeeleza hay oleo Alhamisi mara baada ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Leonard Swai kudai kesi ilipangwa kutajwa, upelelezi wake bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Wakili wa Sethi, Melchisedeck Lutema alieleza kuwa wana maombi na wakaomba upande wa mashtaka waieleze mahakama kwa nini Seth hapelekwi hospitali.

Pia aliomba mahakama nitumie busara na mamlaka yake kuhakikisha mshtakiwa Seth anapelekwa hospitali.

Kwa upande wa wakili mwingine wa upande wa utetezi, Paschal Kamala amesema washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo Juni 19,2017 na kwamba hadi leo Alhamisi ni siku 87, wapo rumande wanakabiliwa na mashtaka yasiyo na dhamana na maelezo ni kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Ameeleza kuwa ili haki ionekane inatendeka kwa wakati kwa upande zote mbili wanaomba upelelezi ukamilike mapema.

Kwa upande wa Wakili Swai yeye aliitarifu mahakama kuwa Seth alipelekwa hospitali na kwamba anatibiwa Magereza na kuna Dk Sotto Pakacha ambaye ni mtaalam anamtibu kila siku akiwa gerezani.

"Nimefuatilia mimi mwenyewe na nimeuona huo utaratibu  hata akiwa na shinikizo la damu (presha) ama akiwa na tatizo lolote anatibiwa,"amesema Swai.

Aliongeza kuwa mshtakiwa Sethi hajawahi kuwasilisha vyeti ama kumbukumbu Magereza kuwa ana tatizo hilo ili daktari aweze kujua anaanzia wapi.

Swai amesema walishampeleka Hospitali ya Amana na alitibiwa na jopo la madaktari akiwamo mmoja anaitwa Erick na kwamba Magereza wapo katika kuchukua vipimo ili afanyiwe MRI. Amri yako imetelezwa alisisitiza kusema Swai.

Amekubali kuchelewa kwa kesi ila wanaendelea na upelelezi kwa kuwa makosa ya kughushi yanahusisha taasisi nyingi ndio maana unachukua muda mrefu.

Wakili Lutema alidai kuwa maelezo ya upande wa mashtaka ni maelezo tu, hayana uthibitisho kwa kuwa suala la kutibiwa ama kutotibiwa ni la mshtakiwa na yupo mahakamani asikilizwe aseme anatibiwa ama hatibiwi.

Pia alieleza kuwa ni wakati wa kutekelezwa kwa amri ya Mahakama iliyosema mshtakiwa akatibiwe katika Hospitali ya Muhimbili  na akaomba mahakama itumie busara na mamlaka yake kuhakikisha amri yake inatekelezwa na Mahakama imeamuru apelekwe hospitali ya Muhimbili,  kesi imeahirishwa hadi Septemba 29, 2017.