Barabara tisa kujengwa Songwe

Muktasari:

Pia amewataka waache fikra za kutofautisha barabara za vijijini na mijini badala yake wazingatie  kuongeza uchumi wa wakazi wa maeneo hayo kwa kuwaboreshea miundombinu ya barabara.


Mbozi. Mkoa wa Songwe na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Nchini (TARURA) wameingia makubaliano kwa kuwekeana saini mikataba tisa ya barabara, madaraja 10 na kalavati 18 vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh1bilioni.

Akizungumza baada ya kuwekeana saini mikataba hiyo, mjini Vwawa leo Februari 7, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa ameitaka Tarura na wakandarasi kutengeneza barabara za vijijini kwa viwango na ubora sawa na mjini.

Pia amewataka waache fikra za kutofautisha barabara za vijijini na mijini badala yake wazingatie  kuongeza uchumi wa wakazi wa maeneo hayo kwa kuwaboreshea miundombinu ya barabara.

Galawa ametaka kuwepo na njia maalumu ya kupitisha mifugo badala ya kuiacha ikipita barabarani na kuziharibu, pia kuwaondoa mapema wote wanaofanya shughuli za kibinadamu katika eneo la hifadhi za barabara.

Mratibu wa Tarura mkoani Songwe, Mhandisi Ernest Mgeni amesema mchakato wa kuwapata makandarasi walioshinda zabuni hiyo ulianza Novemba 13 mwaka jana kwa kutangaza zabuni nchi nzima zenye kazi 21 za matengenezo ya barabara na kuwapata washindani 104.

Amesema hatua ya pili ilikuwa kufanya mchakato wa kuwapata makandarasi ambapo zabuni 9 zilipata makandarasi na nyingine kuendelea katika mchakato huku zabuni nyingine 8 mikataba yake inatarajia kusainiwa baadaye mwezi huu.

Amezitaja barabara zinazotarajiwa kufanyiwa matengenezo kuwa ni pamoja na zitakazofanyiwa matengenezo maalumu, ukarabati na matengenezo ya dharura na mara baada ya kusainiwa mikataba kazi zitaanza baada ya siku 14 na zitafanywa katika kipindi cha miezi minne na chache miezi mitatu.

Meneja wa Tarura Wilaya ya Mbozi, Mhandisi Naftari Chaula amezitaja barabara zinazotarajia kufanyiwa matengenezo katika mji wa Vwawa ambao ni makao makuu ya mkoa wa Songwe ili kupanua sekta ya uchukuzi na usafirishaji na kupunguza msongamano katika mji huu.

Amesema kutokana na ongezeko la vyombo vya usafiri katika mji huo wanatarajia kupanua barabara za Tacri – Ilembo yenye urefu wa kilometa mbili, Ukinga –CCM kilometa 1.5, Ilasi – Ilolo Sekondari kilometa mbili, Lutherani – Sifika kilometa 1.3, Ilolo – Ndolezi kilometa 2 na Ihanda Gharani mita 600.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo aliwataka makandarasi waliopata kazi za ujenzi kuzifanya kwa weledi na uzalendo ili zilingane na thamani halisi ya fedha watakayolipwa.

Mmoja wa makandarasi hao Joseph Mtegwa wa Kampuni ya Kimbunga Enterprises, alisema wanapopata kazi za ujenzi wa barabara vijijini wananchi wanashindwa kuelewa aina ya kazi zinazofanyika kutokana na kutokuwepo uwazi wa mikataba.

Ametolea mfano kuwa wakati mwingine mikataba imekuwa ikitoa fursa kufanyika kazi za mikono kwa wananchi wa eneo husika ili waweze kujipatia kipato, lakini wamekuwa wakidhani wamedharauliwa na kwamba mkandarasi ana lengo la kujipatia faida kubwa kwa kuacha kutumia mitambo.