Binti mwenye uvimbe begani afariki dunia

Muktasari:

Mkurugenzi wa ORCI, Julius Mwaiselage amethibitisha kifo hicho, kwamba taasisi hiyo inaandaa taarifa kamili.

Dar es Salaam. Maria Amrima (17) mkazi wa Mtwara, aliyeanza kupatiwa matibabu Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) jijini hapa kutokana na uvimbe mkubwa begani, amefariki dunia.

Mkurugenzi wa ORCI, Julius Mwaiselage amethibitisha kifo hicho, kwamba taasisi hiyo inaandaa taarifa kamili.

Binti huyo ambaye alitakiwa kufanyiwa upasuaji Muhimbili mwaka mmoja uliopita wakati huo uvimbe ukiwa bado mdogo, alitoweka baada ya kwenda katika tiba za asili kabla ya kurejea hospitalini hapo Januari 3 mwaka huu, baadaye kuhamishiwa katika taasisi hiyo.

Awali jopo la madaktari bingwa kutoka vitengo vitatu vya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Ocean Road, waliungana kwa pamoja kuangalia uwezekano wa kumtibu na kuokoa maisha yake baada ya tiba ya upasuaji kushindikana.