BoT yaonyesha utegemezi wa bajeti wapungua

Muktasari:

  • Ripoti hiyo ya mwaka wa fedha 2016/17 iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita inaonyesha utegemezi huo umepungua kutoka asilimia 3.5 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 mpaka asilimia 1.5.

Mkakati ya Serikali kusimamia ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi yake umepunguza kiasi cha utegemezi wa bajeti kwa asilimia mbili ya Pato la Taifa, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha.

Ripoti hiyo ya mwaka wa fedha 2016/17 iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita inaonyesha utegemezi huo umepungua kutoka asilimia 3.5 ya Pato la Taifa mwaka 2015/16 mpaka asilimia 1.5.

Ripoti inabainisha baadhi ya mambo yalichangia hilo kuwa ni mwenendo mzuri wa ukuaji uchumi kwa asilimia 7.0 mwaka 2016, kuendelea kushuka mfumuko wa bei na ongezeko la makusanyo ya mapato kulifanikiwa kupunguza utegemezi.

Kwenye neno lake katika ripoti hiyo, gavana mstaafu, Profesa Benno Ndulu amesema ukuaji huo wa uchumi kwa miaka mitatu mfululizo ulichangiwa na sekta za ujenzi, usafirishaji na uhifadhi, biashara, mawasiliano na viwanda.

“Hali iliendelea kuwa nzuri mwaka 2017 ikichangiwa na sera ya uchumi wa viwanda, uwekezaji kwenye miradi ya maendeleo na kuimarika kwa uzalishaji na usambazaji umeme,” alisema Profesa Ndulu.

Kwa mwaka huo, gavana huyo alisema mfumuko wa bei ulikuwa tarakimu moja kwa wastani wa asilimia 5.0, ambalo ni lengo la muda mfupi lililojiwekea benki hiyo hali ambayo inatarajiwa kuendelea kuwapo mwaka huu wa fedha pia.

Uhakika huo, anasema unatokana na uhakika wa chakula maeneo mengi nchini. Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha kuanzia Januari mpaka Desemba 2017 mfumuko uliongezeka kwa asilimia 0.1 tu kutoka asilimia 5.2 mpaka asilimia 5.3.

Alipokuwa akiwasilisha ripoti hiyo ya mwaka, mkurugenzi wa sensa na takwimu za jamii wa NBS, Ephraim Kwisegabo alisema:

“Kuna mabadiliko madogo ya wastani wa mfumuko wa bei kati ya mwaka 2017 na 2016. Kwa kiasi kikubwa, mabadiliko hayo yamesababishwa na bei za vyakula vinavyochangia mizania kwa asilimia 38.5.”

Licha ya vyakula, sababu nyingine zitakazoshusha mfumuko huo mwaka huu wa fedha ni sera thabiti za fedha, kushuka kwa bei ya nishati na kutoyumba kwa thamani ya fedha hasa dhidi ya Dola ya Marekani.

Licha ya sekta ya benki kuonekana imetikisika, Profesa Ndulu anasema ipo imara na timamu kwani kuna mtaji na fedha za kutosha kufanikisha mahitaji yaliyopo.

“Kwenye nusu ya pili ya mwaka, sera ya fedha ililegezwa kidogo kukabiliana na changamoto ya ukwasi uliokuwapo. BoT itaendelea kuhakikisha sekta hii haiyumbi, inaboresha mifumo ya malipo na watu wengi zaidi wanatumia huduma za fedha,” alisema.

Marekebisho ya sera yaliyofanywa hasa kupunguzwa kwa riba ya mikopo inayotolewa na BoT kwenda taasisi za fedha kunaelezwa kuwa ni mkakati wa changamoto zilizotokana na Serikali kuhamisha fedha zake kutoka kwenye benki za biashara kwenda Benki Kuu na sera ya kubana matumizi ya Serikali.

Ingawa kanuni za BoT zinaagiza uwiano wa mikopo isiyolipika dhidi ya mikopo ghafi kutozidi asilimia tano, ripoti inaonyesha wastani huo umeongezeka kutoka asilimia 8.7 iliyokuwapo mwaka 2015/16 mpaka asilimia 10.6 mwaka 2016/17.

Hata hivyo, benki hiyo inasema akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kutoka iliyokuwa inatosha kukidhi uagizaji wa bidhaa kwa miezi 4.1 mpaka miezi 5.9.

Mikopo

Ujazo wa fedha ulipungua mwaka 2016/17. Ripoti inaonyesha ujazo huo ulitanuka kwa asilimia 6.0 ikilinganishwa na asilimia 12.7 mwaka ulioishia Juni 2016 kutokana na kupungua kwa mikopo ya sekta binafsi.

Mikopo hiyo iliongezeka kwa asilimia 19.1 mwaka 2016 lakini ilipungua na kuongezeka kwa asilimia 1.2 tu licha ya kutarajiwa kuongezeka kwa asilimia 12.5 mpaka Juni 2017.

Ripoti inaonyesha mikopo ya sekta ya viwanda iliongezeka kwa asilimia 16.6 ikilinganishwa na ilivyopungua kwa asilimia 4.6 mwaka 2016. Mikopo ya biashara pia iliongezeka kwa asilimia 16.1 ikilinganishwa na asilimia 3.5 za mwaka uliopita wakati usafirishaji na uchukuzi ikiongezeka kwa asilimia 22.1.

Mikopo ya wateja binafsi ilipungua kwa asilimia 5.8 baada ya kuongezeka kwa asilimia 36.7 mwaka 2016, sekta ya madini nayo iliongezeka kwa asilimia 12.3 kutoka 32.9.

Hoteli na mighahawa ilikuwa asilimia 7.9 kutoka 18.0 wakati ukandarasi ilikuwa asilimia 5.5 kutoka 10.0 za mwaka 2016.

Mpaka Juni 2016, sekta ya kilimo iliyokuwa na asilimia sifuri, mwaka 2017 ilipungua tena kwa asilimia 0.2.

Mwaka mzima wa fedha, ni Sh206.2 bilioni pekee zilikopeshwana benki za biashara kwenda sekta binafsi.

Umeme

Kwa kuzingatia umuhimu wa nishati kuelekea uchumi wa viwanda, uzalishaji na usambazaji umeme ulikua kwa asilimia 9.1 ikilinganishwa na asilimia 4.4 Juni 2015.

Ongezeko hilo, ripoti inasema limetokana na kukamilika mradi wa Kinyerezi I. kukamilika kwa mradi huo kuliongeza uzalishaji. Zaidi ya kilowati bilioni 6.936 zilizalishwa mwaka 2016 ikilinganishwa na kilowati biloni 6.382 zaa mwaka 2015.

Kwa uzalishaji huo, ilifanya nishati iliyo tayari kwa matumizi, ikijumlishwa na umeme unaonunuliwa kutoka nje, kuongezeka mpaka kilowati bilioni 7.038 mwaka 2016 kutoka kilowati bilioni 6.453 za mwaka uliotangulia.

Kwa sasa, Serikali inatekeleza miradi mingine ya umeme ukiwamo ujenzi wa mradi mkubwa zaidi wa Stigler’s Gorge ambao zabuni yake imeshatangazwa na zaidi ya waombaji 50 kujitokeza.