Bobi Wine ashtakiwa mahakama ya kijeshi

Muktasari:

Bobi inadaiwa kuwa anashikiliwa kwa tuhuma za uchochezi


Uganda. Juzi mwanamuziki Jose Chameleone, alimuombea msamaha kwa Rais Yoweri Museven msanii mwenzake Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’, aliyekuwa akishikiliwa na jeshi la polisi nchini humo.

Hatua hiyo ilikuja ikiwa ni siku moja baada ya dereva wa mwanamuziki huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyadondo Mashariki, kuuawa kwa kupigwa risasi.

Tukio hilo lilitokea katika vurugu za kampeni za ubunge zinazoendelea nchini humo ambapo Bobi anaelezwa kumuunga mkono mgombea huru.

Baada ya tukio hilo, Bobi inadaiwa kuwa anashikiliwa kwa tuhuma za uchochezi, japokuwa Jeshi hilo lilidai kwamba yupo katika matibabu.

Jana mwanamuziki huyo alipandishwa katika mahakama ya kijeshi kwa kukutwa na silaha nzito ambazo kwa kawaida zinatakiwa kumilikiwa na jeshi.

Akisomewa mashtaka yake mbele ya mawakili wake, ilielezwa kuwa Bobi WIne alikutwa na silaha hizo katika chumba cha hoteli.

Mawakili wake wanasema Bobi Wine ameumizwa vibaya na uso wake umevimba kiasi cha kushindwa kuona vizuri.