Bobi: Asanteni kwa kuendeleza mapambano

Muktasari:

Nawashukuru mashabiki na wafuasi wangu kwa kufika hapa kwa ajili ya yangu na familia, mapambano yanaendelea hebu tuendelee na ari hii.” Amesema Bobi.

Wakiso, Uganda. Muda mfupi baada ya kufikishwa nyumbani kwake Alhamisi, Mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi alijitokeza kwenye kibaraza na kuwapungia mkono wananchi na wafuasi ambao aliwashukuru kwa kuendeleza “ari na mapambano” kwa ajili ya kuibadili Uganda iwe bora.
Mwandishi wa gazeti la Daily Monitor Derrick Wandera aliripoti kwamba mbunge huyo maarufu kama Bobi Wine alipungia mikono umati wa watu uliokuwa ukishangilia kwa shangwe. Wananchi walifanikiwa kuwasukuma kando polisi kabla ya Bobi Wine kuhutubia.
“Nawashukuru mashabiki na wafuasi wangu kwa kufika hapa kwa ajili yangu na familia,” alisema Bobi huku akishangiliwa kwa nguvu. Aliongeza: “Mapambano yanaendelea hebu tuendelee na ari hii.”
Umati wa watu uliojaa kwenye eneo nyumbani kwa Bobi Wine ulikuwa ukiimba kaulimbiu yake ya hamasa; People Power, Our Power! Bobi hakuwa anategemea fimbo ya kutembelea kama ilivyokuwa alipokuwa ameachiwa kutoka kizuizini wiki tatu zilizopita. Mkewe Berbie, alikuwa amesimama kando yake.
Baada ya kuzungumza kwa kifupi, Bobi Wine, ambaye alikuwa ametua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe Alhamisi mchana akitokea Marekani, aliondoka na kuingia ndani akisema amechoka na ana njaa na kwamba alihitaji kupumzika.
Kaka yake Eddie Yawe, ambaye alikamatwa na polisi Alhamisi asubuhi alipokuwa akienda uwanjani kumpokea Bobi, alijitokeza kwenye geti la nyumba ya mbunge huyo eneo la Magere, wilaya ya Wakiso, muda mfupi baada ya Bobi Wine kuhutubia.