Bobi Wine awasili Uganda apakizwa kwenye gari la jeshi

Muktasari:

  • Wakati polisi nchini Uganda wakionya mikusanyiko kwa ajili ya mapokezi ya mbunge wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, mwanasiasa huyo leo  Septemba 20, 2018 amewasili nchini humo akitokea Marekani

Kampala. Baada ya kuwasili Uganda akitokea Marekani alipokuwa akipata matibabu, Mbunge  wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amepakizwa kwenye gari la jeshi.

Mara tu baada ya kushuka kwenye ndege ya Kenya Airways, Bobi Wine, alipakizwa kwenye gari ya jeshi na kupelekwa kijijini kwake Magere.

Awali mwanamuziki huyo aliyegeuka mwanasiasa aliapa kukaidi amri hiyo iliyotangazwa mapema akieleza kuwa yeye ni raia huru wa Uganda mwenye haki zote za kutembea kokote hivyo asipangiwe nani ampokee na aende wapi.

Bobi Wine aliyekwenda Marekani kwa ajili ya matibabu baada ya kudai kupigwa na kuteswa wakati akiwa mikononi mwa polisi, amesema kurejea kwake Uganda hakuwahusu polisi, hawapaswi kuhoji nani atampokea.

"Nimekuwa najiuliza kwa nini hawa maofisa wa polisi wanakubali kujidhalilisha kiasi hicho. Wanataka kuamua nani aje kunipokea na wapi nielekee baada ya kuwasili?” Amehoji.

Vyombo vya habari nchini Uganda vimemnukuu msemaji wa polisi, Emilian Kayima aliyewaambia waandishi wa habari kuwa atakapowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Entebbe, mbunge huyo atapokelewa na familia yake na atapatiwa ulinzi kutoka uwanja wa ndege mpaka nyumbani.