Bodaboda marufuku Rufiji kuanzia saa 12 jioni

Muktasari:

  • Usafiri huo umesitishwa kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 12:00 asubuhi.
  • Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Pwani (RCC), Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amesema hatua hiyo inatokana na watuhumiwa wa uhalifu kutumia usafiri huo na matukio hayo kufanyika kati ya muda huo hadi saa mbili usiku.

Kibaha/Rufiji. Kutokana na kukithiri kwa matukio ya uhalifu na mauaji, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani imesitisha usafiri wa bodaboda muda wa jioni wilayani Rufiji.

Usafiri huo umesitishwa kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 12:00 asubuhi.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Pwani (RCC), Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amesema hatua hiyo inatokana na watuhumiwa wa uhalifu kutumia usafiri huo na matukio hayo kufanyika kati ya muda huo hadi saa mbili usiku.

Uamuzi huo umekuja siku mbili baada ya kuuawa kwa mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Ikwiriri Kaskazini, Emmanuel Alberto kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake, tukio hilo likifanya idadi ya viongozi wa Serikali za Mitaa na  polisi waliouawa kufikia takriban 11 katika wilaya za Rufiji na Kibiti

Hata hivyo, Ndikilo amesema Serikali inatambua kuwa hatua hiyo itawaadhiri wengi wasio na hatia wakiwamo wagonjwa ambao wangehitaji usafiri huo kuwawahisha kwenye vituo vya afya, lakini hakuna namna nyingine ya kudhibiti matukio hayo kwa sasa.

“Taarifa za kiintelijensia zinatuelekeza tuanze kusitisha usafiri wa bodaboda Rufiji, licha ya kuwapo matukio kama hayo Mkuranga na Kibiti,” amesema Ndikilo.

Awali, Katibu Msaidizi, Uendeshaji na Utawala wa CCM Mkoa wa Pwani, Mary Nchimbi amesema mauaji hayo yana sura inayofanana lakini chanzo chake hakijaelezwa wala wahusika kukamatwa, huku vyombo vya dola vikiwa kazini, huku Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Pwani, Baraka Mwango akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kushirikisha vyama vyote vya siasa na viongozi wa dini ili kukomesha hali hiyo.