Bodaboda waonyesha ‘jeuri yao’

Waziri wa Afya,Jinsia,Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu

Muktasari:

Msaada huo ulipokelewa na Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalim alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi tatu za watoto katika hospitali hiyo.

Mbeya. Umoja wa Waendesha bodaboda jijini Mbeya, wamechangia mifuko 75 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa wodi za watoto Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya.

Msaada huo ulipokelewa na Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalim alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi tatu za watoto katika hospitali hiyo.

“Niseme nimevutiwa na mchango wa umoja wa waendesha bodaboda, mmefanya jambo jema na la Kizalendo,” alisema Waziri Ummy.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy aliwaagiza waganga wakuu wa mkoa na wilaya nchini, kuhakikisha wanatumia vizuri rasilimali zilizopo maeneo yao  kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili katika utoaji huduma za afya badala ya kusubiri fedha kutoka serikalini.

Awali, akitoa taarifa ya ujenzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk Godlove Mbwanji alisema wodi  hizo zitagharimu Sh300 milioni zinatokana na fedha za hospitali na michango ya wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Mbeya.