Bodi ya pamba yatangaza mikakati yake

Muktasari:

Akizungumza jijini Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Marco Mtunga alisema mikakati hiyo inalenga kuvihakikishia viwanda vya nyuzi na nguo upatikanaji wa malighafi ya kutosha.

Ili kufanikisha lengo la Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, Bodi ya Pamba nchini (TCB), imejipanga kuongeza uzalishaji wa zao hilo hadi tani 300,000 kwa msimu ujao wa kilimo kutoka tani 134,263 msimu uliopita wa 2016/17.

Akizungumza jijini Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Marco Mtunga alisema mikakati hiyo inalenga kuvihakikishia viwanda vya nyuzi na nguo upatikanaji wa malighafi ya kutosha.

“Tunalenga kuendeleza programu ya mafunzo na elimu kwa wakulima kuhusu kilimo chenye tija, kuwahakikishia upatikanaji wa mbegu bora, viuadudu na huduma ya ugani kwa wakati mwafaka,” alisema Mtunga

Kuhusu kukabiliana na upungufu wa maofisa ugani ambao kwa sasa wapo ngazi ya kata, TCB itawatumia wakulima wawezeshaji 4,534 ambao mashamba yao yatatumika kama darasa kutokana na mafanikio na kilimo chenye tija.

Pia, Mtunga alisema kwamba TCB imetenga zaidi ya Sh50 milioni kununulia vipandio vya kukokotwa kwa ng’ombe vitakavyogawanywa kwa wakulima, ili kuwawezesha kupanda kwa mstari na kuongeza idadi ya miche na mavuno.

Pamba hulimwa katika eneo linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa eka milioni moja katika wilaya 45 za mikoa 16 nchini, kwa sasa wakulima wengi huambulia kati ya kilo 200 hadi 300 kwa eka badala ya kati ya kilo 800 hadi 1,200 iwapo wangelima kwa tija.

Katika mikakati hiyo, TCB kwa kushirikiana na wadau wengine itasisitiza kilimo cha mkataba ambacho kimeonyesha ufanisi katika mikoa ya Mwanza na Mara.

“Uzalishaji katika mikoa hii miwili iliyotumia kilimo cha mikataba umeongezeka kutoka tani 12.5 msimu wa kilimo 2015/16 hadi tani 18.8 msimu wa 2016/17,” alisema Mtunga.

Pia, uzalishaji na uandaaji mbegu bora umepewa kipaumbele kwa kutengewa Sh657 milioni kwa ajili ya utafiti katika Chuo cha Utafiti cha Ukiriguru na ujenzi wa Bwawa la Nkanziga linalotumiwa kwa shughuli za kilimo cha mbegu bora wilayani Igunga.

Akizungumzia mikakati hiyo, mkulima Cosmas Ng’wanagwanchele kutoka Nyambiti wilayani Kwimba alishauri halmashauri kutenga fedha kuwezesha maofisa ugani kuwafikia wakulima kwa wakati.