Bogoss kuisindikiza Sikinde miaka 40 ya kuzaliwa

Muktasari:

Sherehe hiyo inatarajiwa kufanyika viwanja vya Bandari Tandika jijini Dar es Salaam 

BENDI ya Bogoss Musica iliyoingia katika burudani kwa kishindo ikiwa chini ya Mwanamuziki, Nyoshi El Saadat, inatarajia kuisindikiza bendi kongwe ya Orchestra Mlimani Park ‘Sikinde’ kwenye sherehe ya kutimiza miaka 40 tangu ilipoanzishwa mwaka 1978.

Sherehe hiyo inatarajiwa kufanyika viwanja vya Bandari Tandika jijini Dar es Salaam Jumamosi ya Septemba Mosi, 2018 na bendi hiyo itatumbuiza nyimbo zake zote tangu ilipoanzishwa.

Akizungumza na MCL Digital, kiongozi wa Sikinde, Mwimbaji Abdallah Hemba amesema, siku hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya furaha, hivyo amewapa nafasi mashabiki kufika kwa wingi na kutoa zawadi mbalimbali kwa wanamuziki vilevile kuburudika kwa nyimbo walizowaandalia.

Aidha Hemba alisema wameichagua Bendi ya Bogoss Musica kuwasindikiza siku hiyo kutokana na mwitikio mzuri ilioupata kwa mashabiki wa muziki wa dansi tangu ilivyozinduliwa mwanzoni mwa mwezi huu.

“Tumeichagua Bogoss Musica ya Nyoshi El Saadat kutusindikiza kutokana na jinsi alivyouamsha muziki wa dansi ilipofanya uzinduzi waka pale Escape One. Imepokewa vizuri na mashabiki, hivyo tumeona tuendeleze kupeana nguvu katika kuurudisha muziki wa dansi pale ulipokuwa au na zaidi,”alisema Hemba.

 

 

“Tumejipanga kuwapa burudani mashabiki wetu, hivyo waje kwa wingi, pia tunawahakikishia tutawaimbia nyimbo tangu kuanzishwa kwa bendi hadi hapa tulipofikia.

Agosti Mosi mwaka huu, Mlimani Park imetimiza miaka 40 tangu ilipoanzishwa na itafanya sherehe zake Septemba Mosi.

 

Kundi hilo linashika nafasi ya pili kwa ukongwe nyuma ya wapinzani wao wa jadi, Msondo Ngoma ambayo imeanzishwa mwaka 1964.

Baadhi ya wanamuziki wakongwe kama vile, Hassan Rehani Bitchuka ‘Stereo’ ambaye ni mwimbaji kiongozi aliyeitumikia bendi hiyo kwa vipindi tofauti na kwa mara ya kwanza alijiunga na Sikinde mwaka1979.

 

Ndani ya bendi hiyo yupo mwanamuziki aliyeandika historia ya kutoihama tangu alipojiunga mwaka 1978, huyo ni Habib Abass Mgalusi ‘Jeff’ ambaye ni mpiga dramu.

Vilevile mpiga tumba wa bendi hiyo, Ally Omar Jamwaka ‘Ally Tumba’ ni miongoni mwa wanamuziki waliofanya kazi na Sikinde tangu mwaka 1982 alipojiunga nayo akitokea bendi ya Washirika.

Wanamuziki wengine wanaounda kundi hilo ni Hemba, Hassan Kunyata, Musemba wa Minyugu na Ismail Msakala hawa ni waimbaji.

Wengine ni Ramadhani Mapesa, Kaingilila Maufi, Mjusi Shemboza na Karama Tony (wanapiga magitaa). Pia, kina Hamis Milambo, Mbaraka Othman na Shaaban Lendi wanatumikia idara ya ala za upulizaji.