Bomoabomoa mpya kutikisa nchi nzima

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akisoma nyaraka wakati alipoenda kutatua mgogoro wa ardhi wa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa eka 12,750. Aliyevaa miwani kulia ni mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelote Stephen. Picha na Wizara ya Ardhi

Muktasari:

  • Waziri William Lukuvi amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji kuweka alama ya “X” na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali.

Dar es Salaam. Wakati ubomoaji wa nyumba zilizo kandokando ya barabara ukiendelea, waliojenga bila ya vibali sasa wajiandae kwa ubomoaji mwingine, kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari ya Wizara wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Waziri William Lukuvi amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji kuweka alama ya “X” na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali.

Agizo hilo, ambalo utekelezaji wake utagusa mamilioni ya watu, pia litatekelezwa kwa majengo yanayojengwa katika viwanja vilivyochukuliwa kwa dhuruma kutoka kwa watu walio na hatimiliki za ardhi.

Kwa takriban miezi minne sasa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) unabomoa majengo yaliyo ndani ya eneo la hifadhi ya Barabara ya Morogoro eneo la Kimara hadi Kiluvya, huku Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) ikibomoa nyumba zilizo kwenye hifadhi ya reli.

Kwa mujibu wa Tanroads, takriban nyumba 1,300 za wananchi wa maeneo hayo zilizojengwa ndani ya mita 121.5 kutoka katikati ya barabara hiyo kwa kila upande zitabomolewa na tayari 1,000 zimebomolewa.

Bomoabomoa hiyo inalenga kuwezesha ujenzi wa barabara ya njia sita ili kupunguza msongamano na hasa Ubungo.

Tanroads pia imeweka alama ya “X” kwenye nyumba za wananchi mkoani Iringa kupisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami itakayoanzia Kijiji cha Tungamalenga ambako ndiko kuna lango la kuingilia Hifadhi ya Ruaha na itakwenda mpaka Iringa Mjini.

Miongoni mwa waathirika wa ubomoaji huo ni Waziri Lukuvi, ambaye alishiriki kuvunja nyumba yake wiki iliyopita.

Nayo Rahco imeweka alama ya kutaarifu kuvunja majengo katika baadhi ya maeneo nchini yaliyojengwa ndani ya hifadhi ya reli.

Miongoni mwa maeneo hayo yapo Dar es Salaam na Morogoro ambako tayari nyumba zimevunjwa. Mikoa mingine ambayo Rahco imeweka alama hizo ni Tanga, Kilimanjaro, Mwanza, Kigoma, Shinyanga na Tabora.

Vilevile, ubomoaji wa nyumba zilizopo kando ya miundombinu ya reli ni agizo la Serikali ambayo inalenga kuiboresha, ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa inayotoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma.

Kuhusu ubomoaji huo mpya, Waziri Lukuvi ametoa agizo kwa wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji kuweka alama ya kutaarifu ubomoaji majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali na pia kwa majengo yanayojengwa kwenye viwanja ambavyo watu wamedhulumiwa.

Lukuvi alitoa agizo hilo alipofanya ziara wilayani Sumbawanga, Rukwa kutatua mgogoro wa ardhi.

Kutokana na urasimu uliokuwepo ofisi za ardhi, watu wengi wamekuwa wakijenga nyumba zao bila ya kupata vibali na hivyo kujikuta ama wamejenga maeneo yasiyoruhusiwa au yaliyoanishwa kwa miradi ya kijamii.

Pia taratibu za gharama za kupata viwanja vilivyopimwa, hukatisha tamaa watu na hivyo kununua viwanja vya asili na kujenga kiholela.

Waziri Lukuvi pia ameagiza eneo la Malonje lililokuwa shamba la mifugo lenye ukubwa wa eka 12,750, lirejeshwe serikalini kwa kuwa utaratibu wa kuligawa umekiukwa na masharti ya uendeshaji hayajazingatiwa.

Taarifa hiyo ya wizara inaeleza kuwa Waziri Lukuvi amesema tatizo la ujenzi holela linaanza pale wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji wanapoacha majengo kuibuka katika miji yao bila kujua ujenzi huo kama una vibali au unajengwa katika viwanja vyenye hati na wahusika wa hati hizo ndio wanaojenga.

“Hatuwezi kuendelea na zoezi la kufanya urasimishaji wa makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo kinajulikana. Kwa hiyo naagiza wakurugenzi, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji kuweka “X” katika majengo yote yanayojengwa bila vibali na ujenzi unaofanywa kwenye viwanja vya watu maskini kwa dhuluma,” alisema Lukuvi.

Alisema atapambana na viongozi pale atakapokuta majengo yasiyo na vibali, yamejengwa kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kujenga au yamejengwa katika viwanja vya watu wengine.

Waziri Lukuvi alisema pia atapambana na viongozi wanaoshindwa kutekeleza uvunjaji wa majengo yaliyowekwa “X” kwa kuwa huo ni uzembe unaotokea nchi nzima.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Stephen aliahidi kufanyia kazi maagizo hayo kikamilifu na kwa haraka ili kuondoa migogoro na kero zinazoukabili mkoa huo katika masuala ya ardhi.

Wakati huohuo, Lukuvi amesema Serikali inakusudia kuwanyang’anya mashamba watu wote waliopata mikopo kwa kuyatumia kama dhamana kutoka benki za ndani na nje, lakini fedha walizopata hazitumiki kuinufaisha nchi wala kuiendeleza ardhi hiyo.

Alisema wapo wawekezaji waliotumia mashamba kupata mikopo, lakini fedha wanazopata huzitumia kuwekeza nchi za Ulaya, Dubai na kwingine duniani.

“Haiwezekani mtu atumie ardhi yetu kujipatia fedha halafu azitumie kuendeleza nchi nyingine na kuiacha ardhi yetu kama pori, jambo ambalo linaleta migogoro mikubwa katika jamii inayoyazunguka maeneo hayo,” alisema.

“Kwa hiyo wizara imekusudia mwezi ujao kupeleka bungeni marekebisho ya Sheria Namba 24 ya mwaka 1999 ili kuongeza vifungu ambavyo vitadhibiti mikopo inayopatikana kwa kutumia ardhi kama dhamana.”

Lukuvi amesema kuanzia Novemba 2017 tatizo hilo litakwisha kwa kuwa jukumu hilo zitapewa benki na wakopeshaji ambao watafuatilia kwa karibu maombi ya mikopo kutokana na mpango mkakati uliowasilishwa katika benki husika.

“Kama benki husika haitawafuatilia na kuamua kumuachia mtu huyo kwa kuwekeza fedha hizo anavyotaka bila kuendeleza ardhi husika, Serikali itamnyang’anya mkopeshwaji shamba hilo kwa kuwa atakuwa amekiuka sheria halafu benki ambayo itamuachia mtu achukue fedha na asiendeleze shamba lile itakuwa imekula hasara,” alisema.