Bomoabomoa ‘yafutika’ Tanga

Muktasari:

  • Maofisa wa Rahco wamefuta alama za X walizoweka kwenye nyumba zilizo karibu na reli.

Homa ya wamiliki wa nyumba zilizowekwa alama ya X jijini Tanga imeanza kupoa baada ya maofisa wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), kupita mara ya pili na kuandika maneno imefutwa.

Ofisa Habari wa Rahco, Catherine Moshi amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya uongozi wa kampuni hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella kufikia uamuzi kwamba busara itumike ili Jiji la Tanga lisitoweke.

“Maofisa wetu wapo jijini Tanga wanapita kufuta alama ya X kwenye nyumba zilizo kwenye mapishano ya reli ziliwekwa kwa umbali wa mita 100 na sasa itapungua hadi mita 30,”amesema Moshi.

Moshi amesema katika kikao na Shigella ilibainika isipotumika busara na sheria ya kubomoa nyumba zote zilizo umbali wa mita 100 ikifuatwa kwenye makutano ya reli, basi mji wa Tanga utatoweka na kubakiwa na nyumba chache.

Amesema kutokana na hilo, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) italazimika kuweka taa kubwa na vibao vyenye alama kuonyesha kuwa ni makutano ya reli.

Ofisa huyo amesema sehemu nyingine yatajengwa mageti na watakuwepo watumishi wenye bendera kuonyesha ishara wakati treni itakapokuwa ikipita.

 

Mwananchi Digital imeshuhudia baadhi ya nyumba katika mitaa ya Chuda na Central jijini Tanga ambazo  zilikuwa zimewekwa alama ya X zikiwa na maandishi ya njano yanayosomeka imefutwa.

Mkazi wa Chuda, Omari Jumaa amesema busara imewaokoa baadhi ya wenye nyumba, lakini bado kuna hofu kwa wengine.