Bomoabomoa Kibaha kuanza Novemba 24

Muktasari:

Bomoabomoa hiyo itawahusu wakazi ambao majengo yao yamo ndani ya mita 60 kila upande wa barabara na ambao tayari nyumba zao zimewekewa alama ya ‘X’ kuwataarifu kuwa wamejenga sehemu isiyo sahihi.

Kibaha. Wakazi wa Kiluvya, Mailimoja hadi Tamko Kibaha waliojenga ndani ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro, wametakiwa kubomoa majengo yao kabla ya bomoabomoa kuanza Novemba 24.

Bomoabomoa hiyo itawahusu wakazi ambao majengo yao yamo ndani ya mita 60 kila upande wa barabara na ambao tayari nyumba zao zimewekewa alama ya ‘X’ kuwataarifu kuwa wamejenga sehemu isiyo sahihi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema katika kikao cha Bodi ya Barabara kuwa wananchi watambue kuwa taarifa walizopewa za kubomolewa nyumba zao ni za kweli na shughuli hiyo itahusu nyumba zilizo ndani ya mita 60 kila upande na siyo mita 120 zilizotangazwa awali.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Tumaini Sarakikya alisema tangazo la awali lililoeleza kuwa bomoabomoa hiyo, itakayokumba pia soko, itahusu majengo yaliyo ndani ya mita 120, halikueleweka vyema, bali ni mita 60 kila upande.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Jenifa Omolo alisema maandalizi ya kuwahamisha wafanyabiashara wa Soko la Mailimoja yanaenda vizuri na wametoa maombi maalumu ili kituo kikuu cha mabasi cha Mailimoja kiendelee kubaki kwa muda eneo hilo wakati mchakato wa kuanza ujenzi wa kituo cha kisasa ukiendelea chini ya ufadhili wa Benki ya TIB.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpta Mshama alitumia muda mrefu kuwakingia kifua wananchi hasa wafanyabiashara wa soko la Mailimoja wasiondolewe kwanza kabla Tanroads haijajua italitumia vipi eneo hilo na kwamba halmashauri haijaweka miundombinu kwenye eneo wanakohamishiwa.

“Mimi bado naona tunawasumbua hawa wananchi wakati hawana tabu ya kuondoka. Wote waliowekewa ‘X’ wanajua siku yeyote wanatakiwa kuondoka,” alisema.

“Lakini napata tabu kwa nini tunawaondoa hasa wafanyabiashara wa soko huku hatujawaandalia mazingira mazuri. Tanroads mmekua mnabomoa maeneo mengi tu lakini hamyaendelezi wakati mwingine huwa mapori, sasa kwa nini msisubiri kwanza?”