Bomoabomoa ilivyopeleka kilio kwa wazee

Muktasari:

  • Hawa ni wazee walioathiriwa na bomoabomoa iliyotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ikilenga upanuzi wa Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya.

 Wengi wamepoteza tumaini, wakiomboleza wakihoji waende wapi?

Hawa ni wazee walioathiriwa na bomoabomoa iliyotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ikilenga upanuzi wa Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya.

Bomoabomoa hiyo iliyoanza Juni, inahusisha nyumba zilizo ndani ya mita 121.5 kila upande kutoka katikati ya barabara hiyo.

Waandishi wetu ambao wamekuwa wakifuatilia operesheni hiyo, walizungumza na wazee wapatao 70 walioathiriwa na bomoabomoa baadhi yao wakiwa wagonjwa, wenye ulemavu na wengine wakiwa hawajiwezi kiuchumi.

Miongoni mwao ni Athuman Kigongo (90) na mkewe Mwajuma Nguzo (70) ambao hivi sasa wamepata hifadhi katika nyumba ya Hadija Hussein (60) Mbezi kwa Yussufu.

“Sisi ni binadamu, leo kwa hawa wenzangu kesho inaweza kuwa kwangu, nitawasitiri kwa miezi miwili,” alisema Hadija.

“Tulikuwa na nyumba mbili pale (Kwa Yussufu), moja tulipangisha tukawa tunapata fedha ya kuendesha maisha yetu, sasa hivi hatuna chochote tupo hapa kwa huyu msamaria mwema lakini hatuna chakula. Tunaomba Serikali itusaidie chakula na mahali pa kuishi hatuna msaada,” alisema Mwajuma.

Jirani yao mwingine, Ally Athuman (66) ambaye hivi sasa anauguza majeraha baada ya kuvunjika mguu na mkono alipokuwa akiondoa mabati ili yasiharibiwe na tingatinga lililokuwa likibomoa nyumba yake hivi sasa anaishi kwa mtoto wake ambaye nyumba yake haikuathiriwa.

Mzee Athuman, baba wa watoto 12 na wake watatu amepoteza nyumba nne.

Waandishi wetu pia waliwatembelea Anselimi Temba (82), James Shilinde (80), John Mlangi (78) na Zainabu Mwinyimvua (84), Samwel Manyota (75) na mke wake Lucy Manyota (66) ambao nyumba zao zimewekewa alama ya X huku wenyewe wakikabiliwa na maradhi mbalimbali ikiwamo, saratani, pumu, akili na ulemavu.

Wenzao, Abdul Saukonde (78) na Azaria Mnyera (85) wanalala nje baada ya nyumba zao kubomolewa huku wakisema wanasubiri huruma ya Rais John Magufuli.

Alipoulizwa kuhusu msaada kwa wazee hao, mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za wazee la Help Age International, Smart Daniel alisema shirika hilo linaendesha programu zake kwa kutegemea wahisani, “Ingekuwa ni janga limetokea sawa, lakini hili ni mpango wa Serikali, hata tukipeleka kwa wahisani ni kama tunapinga mipango ya Serikali. Ninachoomba kama Taifa tuwe na ubinadamu katika hili.”

Alisema licha ya utekelezaji wa sheria, ipo haja ya kuwanusuru wazee hao.

“Jukumu la Taifa ni kulinda makundi ya watu ambao hali zao ni tete. Hawa ni wazee, watoto na kina mama,” alisema.

Alisema wazee hao wasiachwe hivyo hivyo kwa kuwa hawana uwezo tena wa kujenga makazi mapya kutokana na ukweli kwamba hawana tena njia za kuwaingizia kipato kama ilivyokuwa awali.

“Tukiwaacha hivi maana yake nini? Ni lazima kama Taifa tuweke ubinadamu ili tuone namna gani tunaweza kuwasaidia wazee hawa,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ubungo, Salim Msuya alipoulizwa kuhusu wazee hao alisema, “Bado tunafanya tathmini kujua ni wazee gani wanastahili kusaidiwa maana kuna wengine wana ndugu wa kuwasaidia.”