Sunday, August 13, 2017

Bomoabomoa inavyowatesa wakazi Barabara ya Morogoro

 

By Jackline Masinde, Mwananchi jmasinde@mwananchi.co.tz

Wakati wakiwa kwenye tafakuri ya wapi pa kwenda baada ya makazi yao kuwekewa alama ya X, wakazi wa Kimara, Mbezi na Kiluvya wanaoishi kandokando ya Barabara ya Morogoro wiki iliyopita walikumbwa na janga jingine la kukatiwa huduma muhimu za umeme na maji ili kupisha ubomoaji wa nyumba hizo.

Chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Serikali ina mpango wa kuipanua barabara hiyo kuanzia Kimara hadi Kiluvya, hivyo nyumba zilizopo ndani mita 121.5 kila upande, zinatakiwa kubomolewa.

Uwekwaji wa alama ya X katika majengo yaliyo ndani ya hifadhi ya barabara hiyo ulianza Mei 2 kwa Tanroads kutoa notisi kwa wakazi wa eneo hilo ikiwataka hadi kufikia Juni 8 wawe wamebomoa nyumba zao.

Hali hiyo ilipingwa na wakazi wengi, baadhi wakisema zinazopaswa kubomolewa ni zile zilizo ndani ya mita 30 kila upande wakisema ni 60 na kwamba mita 121.5 ni kubwa mno. Kutokana na utata huo, wapo ambao wamefungua kesi mahakamani.

Mbali na wananchi hao kukimbilia mahakamani wakiamni huko ndiko haki yao itapatikana, bado wameendelea kushuhudia baadhi ya nyumba zikiendelea kuwekewa alama ya X na jipya ni hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), kuwakatia umeme na maji, mtawalia.

Waandishi wa wetu walioweka kambi ya wiki nzima wakiripoti yanayojiri katika eneo hilo, walibaini kuwa nyumba za ibada 30 zimewekewa alama ya X na majengo mengine yakiwa ya kifahari. Miongoni mwa majengo hayo, limo la Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kwa jina la kisanii ‘Profesa J.’

Pia, vituo vya vitano afya, sita vya mafuta, kituo kimoja cha watoto yatima, cha polisi kimoja na ofisi ya Kata ya Msigani, zinasubiri siku na saa tu ya kubomolewa.

Hilo si jambo rahisi kuhimili, baadhi ya wananchi ambao wamefikwa na janga hili hasa wazee wamepata maradhi kutokana na mshtuko na wengine kuishi maisha ya hofu.

Miongoni mwao ni Nicomed Leo (61), mkazi wa Kimara Stop Over ambaye nyumba yake ya ghorofa moja yenye thamani ya Sh900 milioni imewekewa alama ya X.

Leo kwa sasa analala sakafuni huku akiwa amefungia vitu vyake vingine ndani ya magari yake mabovu akisema hana mahali pa kwenda.

Mwingine ni mjane Joyce Elias (70), pia wa Kimara Stop Over ambaye anaishi na wajukuu watano wanaomtegemea katika nyumba yake ya vyumba sita yenye thamani ya Sh60 milioni naye akisema hana pa kwenda.

Familia nyingine ni ya Jonas Lyimo (75) ambayo kwa sasa inaishi maisha ya shida baada ya kumpoteza mpendwa wao, Annacel Lyimo (47) siku ambayo nyumba yao iliwekewa alama ya X.

Ukiacha hao, pia yupo Zainabu Mwinyimvua (84) wa Kimara Stop Over, mjane anayeishi na mtoto wake ambaye ni mlemavu Idd Salehe (54) katika nyumba yao ya tope iliyochakaa huyu naye akisema hana pakwenda.

Wengine ambao wamekuwa wakihangaika huku na huko ni mstaafu John Mlangi (74), ambaye anasema bomoabomoa hiyo imemtia maradhi huku akiapa kwamba hataondoka katika nyumba yake na yuko tayari kuzikiwa humohumo akidai kuwa ndilo kaburi lake.

Mwingine aliyefikwa na fadhaa hiyo ni Revy Kapinga, mjane ambaye ghorofa lake la vyumba 50 likiwa na fremu 30 linatakiwa kubomolewa. Mwenyewe anasema huo ndiyo urithi pekee alioachiwa na mumewe ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uchumi na Kilimo la Chama cha Mapinduzi (Sukita), marehemu John Kapinga kuendesha maisha yake.

Mjane huyu alionyesha hisia zake mbele ya waandishi baada ya kulia mbele ya kaburi la mumewe huku akiomba kwenda kugalagala kwa Rais John Magufuli ili amuonee huruma na kumwachia ghorofa lake.

Wahenga walisema, ukiona mwenzake ananyolewa nawe tia maji. Hali hiyo ndiyo inayomkabili Mzee Anselimi Nere (82). Huyu nyumba yake haijawekewa alama ya X lakini amekuwa akiishi maisha ya hofu baada ya majirani zake kuwekewa alama hiyo. Hivi sasa mzee huyo anaishi kwa tabu kwani wapangaji wake wanne wamegoma kumlipa kodi wakihofia bomoabomoa.

Wiki yote iliyopita, operesheni ya kukata umeme na maji ilipambamoto na hali hiyo iliwaweka wananchi hao katika wakati mgumu kwani waliishi kwa wasiwasi. Kila walipoona gari la polisi, Tanesco, Tanrods au tingatinga, walihaha na kuanza kuokoa vitu vyao wakijua ile saa imewadia.

Wananchi waishi gizani

Katika bomoabomoa hiyo waandishi wetu pia walishuhudia kaya katika zaidi ya nyumba 200 zikiwa hazina umeme baada ya Tanesco kung’oa mita zao wakihofia kwamba zitaharibiwa wakati wa ubomoaji.

Lakini Tanesco hawakutimiza kazi hiyo kirahisi, wafanyakazi wake walipata misukosuko na baadhi walionja hasira za wananchi hao ambao waliwafukuza na kuwatupia vifaa vyao.

Kwa mfano, Jumanne ya Agosti 7, wafanyakazi hao walifika katika nyumba ya Mzee Leo kwa lengo la kukata umeme lakini baadhi ya wananchi waliitana na kujikusanya kisha kuwakabili na kuwafukuza.

Mkono wa Dola ni mrefu, jitihada zao hazikufua dafu kwani baada ya kutimuliwa, wafanyakazi hao walikwenda kuomba msaada wa Polisi na kurejea katika eneo hilo kutimiza azma yao hiyo.

Hatua ya kukatiwa umeme sambamba na maji iliwakatisha tamaa baadhi ya wakazi hao hasa wafanyabiashara ambao wanaotegemea zaidi nishati hiyo ambao waliamua kuondoka.

Miongoni mwa walioamua kuondoka mapema ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kibamba na Mbezi Luis.

Jumamosi ya Agosti 5, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aliongoza ibada maalumu ya kuondoa wakfu wa Kanisa la KKKT Usharika wa Kibamba.

-->