Bosi Necta ashambuliwa baada ya gari alilopanda kusababisha kifo

Katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Charles Msonde

Tabora/Dar. Katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Charles Msonde ameshambuliwa na kujeruhiwa na wananchi baada ya gari alilokuwa amepanda kugonga pikipiki na kusababisha kifo cha dereva.

Tukio hilo lilitokea juzi saa kumi jioni katika Kijiji cha Inala, Kata ya Ndevelwa katika Manispaa ya Tabora.

Akizungumza na Mwananchi jana, Dk Msonde alisema anaendelea vizuri na kwamba ajali ilitokea akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kazi.

“Ninaendelea vizuri. Haya maumivu ninayoyasikia yanatokana na kipigo kutoka kwa wananchi waliotuvamia baada ya ajali ile kutokea,” alisema Dk Msonde.

Hata hivyo, katibu mtendaji huyo hakuwa tayari kueleza kwa kina chanzo cha ajali na namna walivyoshambuliwa. “Naomba itoshe kusema ninaendelea vizuri.”

Ofisa habari wa Necta, John Nchimbi alisema Dk Msonde aliruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kidete jana alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tabora, Nestory Didi alisema gari alilopanda Dk Msonde lilimgonga Mzee Salum (23) alipokuwa akikata kona kuingia nyumbani kwake.

Alisema kutokana na ajali hiyo wananchi walifanya vurugu ndipo dereva alipokimbia na kumwacha Dk Msonde.

Didi alisema Dk Msonde alitibiwa na kuruhusiwa na hakuwa na madhara makubwa mwilini kama baadhi ya watu wanavyodai.

Kamanda huyo aliwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake waache sheria ichukue mkondo wake.

Baadhi ya wananchi katika eneo la tukio walisema Dk Msonde asingeokolewa angepata madhara zaidi.

“Kwa kweli dereva alikuwa na makosa kwani alimgonga kwa nyuma (dereva wa pikipiki) nadhani alifikiri angewahi kukata kona,” alisema Ibrahim Said.

Diwani wa Ndevelwa ilikotokea ajali, Seleman Maganga alisema taarifa alizopewa ni kuwa wananchi walimpiga mwanamke aliyedaiwa kupewa lifti na dereva wa gari hilo.

Alisema hakuwa anafahamu kama Dk Msonde alikuwa kwenye gari lililopata ajali na amempa agizo ofisa mtendaji wa kata afuatilie.

Diwani huyo alisema taarifa alizopewa ni za ujanjaujanja. “Huwa wananchi wananipa taarifa mapema lakini katika hili, hawanipi taarifa kikamilifu nadhani wanaogopa kuwa watuhumiwa,” alisema.

Maganga alisema Salum aliyekufa katika ajali hiyo anatarajiwa kuzikwa mjini Tabora na alikuwa akiishi jirani na Shule ya Msingi Inala.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo jana, mganga mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Gunini Kamba alisema yupo kwenye mkutano.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa naye alisema yupo kikaoni, lakini alieleza kuwa na taarifa za ajali hiyo.

Gari lililohusika katika ajali hiyo mali ya Serikali jana lilikuwa limeegeshwa kituo cha polisi.