Bosi mpya Jeshi la Magereza aanza kulisuka

Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali Phaustine Kasike

Muktasari:

Jana, Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali Phaustine Kasike alifanya mabadiliko ya kiuongozi kwa kuwateua wakuu wapya wa Magereza wa mikoa ya Tanzania Bara (RPO) 19, huku akiwaacha saba kwenye nyadhifa zao. Ofisa habari wa jeshi hilo, Deodatus Kazinja katika taarifa yake, alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuboresha utendaji.

Dar es Salaam. Zikiwa ni takriban siku 116 tangu Rais John Magufuli kumpa maagizo Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali Phaustine Kasike kufumua jeshi hilo bila kumuonea mtu, jana alitekeleza agizo hilo.

Julai 14 wakati wa hafla fupi ya kumuapisha iliyofanyika Ikulu jijiini Dar es Salaam, Rais Magufuli alitumia dakika 20 kueleza mambo asiyopendezwa nayo ndani ya jeshi hilo na kumtaka kuyafanyia kazi kwa kulisuka upya.

Jana, Kamishna Kasile alifanya mabadiliko ya kiuongozi kwa kuwateua wakuu wapya wa Magereza wa mikoa ya Tanzania Bara (RPO) 19, huku akiwaacha saba kwenye nyadhifa zao. Ofisa habari wa jeshi hilo, Deodatus Kazinja katika taarifa yake, alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuboresha utendaji.

Alisema Kasike amewateua na kuwathibitisha maofisa sita kuwa wakuu wa vyuo vya Magereza na kuwabadilisha watatu katika vitengo muhimu.

Kazinja alisema mabadiliko hayo yamewagusa wakuu wa Magereza wa mikoa ya Katavi, Songwe, Njombe, Simiyu na Geita ambayo ilikuwa haina uongozi wa kimagereza katika ngazi hiyo.

Walioteuliwa kwenye mikoa hiyo ni Alexander Mmassy (Katavi), Lyzecky Mwaseba (Songwe), Festo Ng’umbi (Njombe), Robert Rumanyika (Geita) na Andulile Mwasampeta (Simiyu). Pia, Alexander Nyefwe (Ruvuma) na Leonard Burushi (Kigoma) wameteuliwa kushika nafasi hizo kufuatia waliokuwapo katika mikoa hiyo kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Aliwataja waliobaki katika nafasi zao kuwa ni Mkuu wa Chuo KPF, Lazaro Nyanga; Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwawani, Anthony Sogoseye na Msaidizi wa Mkuu wa Chuo Ruanda, Enock Mwanguku ambaye kwa sasa anakuwa mkuu wa chuo hicho.

Wengine ni kaimu RPO katika vyuo mbalimbali na wengine wamethibitishwa ambao ni Hasseid Mkwanda (Iringa), Anderson Kamtearo (Arusha), Emmanuel Lwinga (Tanga), Masudi Kimolo (Manyara), Joel Matani (Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji), Rehema Ezekiel (Pwani), Msepwa Omary (Singida) na Ally Uwesu (Mkuu wa Kikosi Maalumu cha Magereza).

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Hamis Nkubasi aliyekuwa Dar es Salaam amehamishiwa makao makuu (ujenzi) na nafasi yake kuchukuliwa na Julius Ntambala, huku Salum Hussein akibaki (Dodoma) na Mkuu wa Chuo Kiwira, Luhende Makwaia anakuwa mkuu wa Magereza Mbeya na nafasi yake kuchukuliwa na Mathias Mkama ambapo Kijida Mwakingi aliyekuwa Mbeya anakwenda makao makuu (Tehama).

Ismail Mlawa aliyekuwa Mtwara amerudishwa makao makuu (Mipango) na nafasi yake kuchukuliwa na Varisanga Msuya aliyekuwa kaimu boharia mkuu wa Jeshi ambako nafasi yake inachukuliwa na Robert Masali anayekuwa Bohari Mkuu wa Jeshi la Magereza.