Bulembo ahofia fedha za korosho kuiangusha CCM

Mbunge wa kuteuliwa (CCM), Abdallah Bulembo

Muktasari:

Ataka wakulima wa korosho kulipwa kwa kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, CCM ilipata kura kwa tabu

Dodoma. Mbunge wa kuteuliwa (CCM), Abdallah Bulembo ameiangukia Serikali akiitaka ipeleke fedha za wakulima wa korosho kwa maelezo kuwa isipofanya hivyo itawagharimu katika chaguzi zijazo.

 

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi ya chama tawala ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 21, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2018/19, bungeni mjini Dodoma.

 

“Pelekeni haraka fedha za korosho jamani. Mnapotaka kuua zao la korosho, pamba na kahawa kwa wakulima mnawaza nini? Hivi hiyo hela ni yetu kweli? Hiki ni chao wapeni,” amesema Bulembo.

 

Amesema kazi iliyofanywa katika mikoa ya kusini hadi kuhakikisha CCM inapata kura ilikuwa ngumu.

 

 “hHivi hamjui kilichotokea Mtwara kweli au mmeweka pamba masikioni?”amehoji.

 

Meneja huyo wa kampeni za Rais John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ametahadharisha kauli ya mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Seleman Bungara maarufu Bwege ya kutishia maandamanoo iwapo Serikali haitatoa fedha za wakulima, akibainisha kuwa si ya kubeza.

 

Jana, Bwege katika mjadala huo alisema maandamano yatafanyika endapo Serikali haitatoa asilimia 65 ya fedha za mauzo ya korosho nje ya nchi kwa wakulima wa mikoa ya Kusini hadi kufikia Juni 30.

 

Katika hoja yake Bwege alisema atahamasisha maandamano ya wabunge na wakulima akimuomba Spika Job Ndugai kuyapokea.