Bulembo amwomba Rais Magufuli kuwakumbuka

Muktasari:

Amemwomba Rais aikumbuke jumuiya hiyo kwenye uteuzi wa nafasi mbalimbali

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Alhaj Abdallah Bulembo amemwomba Rais John Magufuli kuwakumbuka wanachama wa jumuiya hiyo katika nafasi za uteuzi.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumanne Desemba 12, 2017 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete kwenye Mkutano Mkuu Taifa wa Tisa wa Jumuiya hiyo utakaofanyika kwa siku mbili mjini Dodoma. 

Bulembo amesema jumuiya hiyo ina wanachama wenye uwezo, wasomi na wanaoweza kumsaidia Rais katika utekelezaji wa ilani ya chama hicho kupitia nafasi mbalimbali.

Bulembo ambaye leo Jumanne atakabidhi nafasi hiyo kwa mwenyekiti mpya, amemwomba Rais kuangalia uwezekano wa jumuiya hiyo kutoa majina ya wanachama watakaopendekezwa kuwa miongoni mwa wabunge wa kuteuliwa.

Mbali na nafasi hiyo ya upendeleo, Bulembo alimwomba Rais akumbuke pia katika nafasi nyingine za uteuzi wa wakuu wa wilaya na mikoa nchini.

"Lakini hata nafasi za MaDC ni wachache, MaRC tunaye mmoja tu kwenye jumuiya, makada ni wengi angalia na huku kwenye jumuiya ya wazazi," amesema Bulembo.