Bunge ‘Live’ yawagawa wabunge

Muktasari:

Katika misimamo hiyo,  baadhi ya wabunge wa upinzani wamesema  hali hiyo imechangia vikao vya Bunge kupoteza ushawishi, wananchi kutopata taarifa kwa uwazi kuhusu udhaifu unaoibuliwa na wabunge wao na kufifisha wabunge wenye vipaji.

Dar es Salaam. Ikiwa ni mwaka mmoja tangu Bunge liamue kutorusha matangazo ya vikao vyake moja kwa moja kwenye televisheni, imebainika kuwa uamuzihuo bado umewagawa wabunge kulingana na itikadi zao.

Katika misimamo hiyo,  baadhi ya wabunge wa upinzani wamesema  hali hiyo imechangia vikao vya Bunge kupoteza ushawishi, wananchi kutopata taarifa kwa uwazi kuhusu udhaifu unaoibuliwa na wabunge wao na kufifisha wabunge wenye vipaji.

Wakati wa upinzani wakisema hivyo, wale wa CCM wamesema hakuna athari zozote zilizojitokeza kwa kuwa umaarufu wa wabunge au hoja zao hautokani na michango yao kuonekana kwenye runinga.

Pia, wabunge wa upinzani walisema athari nyingine ni kutojipambanua siasa za wabunge wapya na wa zamani, wakiwamo wa CCM ambao wamekuwa wakilalamika chinichini kuhusu kuzuiwa matangazo hayo.