Bunge latenga Sh121 bilioni za matumizi

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango

Muktasari:

Hata hivyo, mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Lucy Magereli amesema hakuna ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Bunge kwa kuwa mambo mengi yanakwama kutokana na kutokutolewa fedha kwa wakati na kufanya wabunge kushindwa kutimiza majukumu yao.

Dodoma. Bunge limetenga Sh121 bilioni kwa matumizi ya mwaka 2017/18 kutoka Sh99 bilioni zilizotengwa mwaka 2016/17.

Hata hivyo, mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Lucy Magereli amesema hakuna ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Bunge kwa kuwa mambo mengi yanakwama kutokana na kutokutolewa fedha kwa wakati na kufanya wabunge kushindwa kutimiza majukumu yao.

Katika swali la nyongeza bungeni jana, alisema kumekuwa na mipango kwenye makaratasi ndani ya Bunge, lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu.

Katika swali la msingi, Magereli alisema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano kumekuwa na mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa shughuli za Bunge ikiwamo kupunguza muda.

“Bunge sasa hukaa kwa siku 10 hadi 12 tu, jambo ambalo linasababisha muda wa kuchangia na mawaziri kujibu hoja kuendelea kupunguzwa hadi kufikia dakika tano kitu ambacho kimepunguza ufanisi wa chombo hicho chenye majukumu muhimu,” alisema.

Mbunge huyo alisema kanuni za Bunge zinaelekeza muda wa kamati kuelekea bajeti ni wiki tatu lakini safari hii wiki moja imepunguzwa.

Akijibu swali la msingi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema mpango wa Serikali kuliwezesha Bunge kufanya shughuli zake kwa ufanisi ni kutoa fedha kutoka mfuko mkuu wa Serikali kwenda kwenye mfuko wa Bunge fungu 40 kwa kuzingatia bajeti iliyoaishinishwa na Bunge.

Dk Mpango alisema taarifa ya utekelezaji ya mfuko wa Bunge na hali ya upatikanaji wa fedha kifungu cha 45 (b) cha Sheria ya Bajeti kinaelekeza hivyo na ndivyo wakatakavyokuwa wakifanya.