Bush asema kuna ushahidi Urusi iliingilia uchaguzi

Muktasari:

Mashirika ya intelijensia ya Marekani yalihitimisha uchunguzi wao kwa kusema Urusi iliingilia uchaguzi wa 2016 ili kumsaidia Trump kushinda. Chunguzi kadhaa zinafanyika zaidi ili kubainisha kama kampeni za Trump zilisaidiwa na Ikulu ya Urusi, Kremlin.


Abu Dhabi, UAE. Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush amesema kuwa "kuna ushahidi wa wazi kwamba Warusi waliingilia" uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka 2016, akimpinga kwa nguvu Rais wa sasa Donald Trump anayekana Urusi kujaribu kuathiri kura.

Japokuwa hakumtaja Rais Trump kwa jina, Bush alionekana kurejea nyuma namna Trump alivyokuwa anahaha kuanzisha uhusiano mzuri na Urusi, pamoja na maoni yake juu ya uhamiaji.

Ikulu ya White House haijasema lolote kuhusu kauli hiyo ya Bush.

"Kuna ushahidi wa wazi kuwa Warusi waliingilia kati," Bush alisema katika hotuba yake Alhamisi akiwa Abu Dhabi, Falme za Kiarabu (UAE). "Kujua kama waliathiri matokeo hilo ni suala jingine."

Bush pia alisema kuwa "ni tatizo kuona taifa la nje linahusika katika mfumo wetu wa uchaguzi. Demokrasia yetu inakuwa nzuri pale watu wanapoyaamini matokeo."

Mashirika ya intelijensia ya Marekani yalihitimisha uchunguzi wao kwa kusema Urusi iliingilia uchaguzi wa 2016 ili kumsaidia Trump kushinda. Chunguzi kadhaa zinafanyika zaidi ili kubainisha kama kampeni za Trump zilisaidiwa na Ikulu ya Urusi, Kremlin.

Trump amekuwa akikana mara kwa mara kuwa na "ushirikiano" wowote na Urusi.

Akimzungumzia Rais wa Urusi, Vladimir Putin, Bush alimwita ni "sifuri."  "Ana kifaa kwenye bega lake," alisema Bush juu ya Putin. "Sababu inayofanya atende haya ni kwa sababu ya kuparaganyika kwa uliokuwa Umoja wa Kisovieti bado kunamsumbua. Kwa hiyo, hatua nyingi anazochukua (ni) kurejesha mamlaka iliyonayo Soviet."

Bush pia alisisitiza haja ya kuunga mkono NATO na washirika wengine wa Marekani duniani.

Putin "anasukuma, daima anasukuma, anachunguza udhaifu," rais wa zamani alisema. "Ndiyo maana NATO ni muhimu sana."

Bush pia alishutumu uamuzi wa Trump wa kufuta mpango ulioanzishwa na utawala wa mtangulizi wake Barack Obama unaowawezesha wahamiaji vijana kuishi Marekani japo kinyume cha sheria ambao walipelekwa ili wabaki Marekani.