Bweni la wasichana lateketea Manyoni

Muktasari:

  • Hilo ni bweni la shule pekee wilayani Manyoni yenye kidato cha tano na sita.
  • Akizungumza muda mfupi baada ya kukagua bweni hilo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe ameagiza timu maalumu iundwe kubaini chanzo cha moto huo.

Manyoni. Bweni la Wasichana la Shule ya Sekondari Mwanzi wilayani Manyoni, Mkoa wa Singida, limeteketea kwa moto na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh50 milioni huku wanafunzi 42 wakinusurika.

Hilo ni bweni la shule pekee wilayani Manyoni yenye kidato cha tano na sita.

Akizungumza muda mfupi baada ya kukagua bweni hilo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe ameagiza timu maalumu iundwe kubaini chanzo cha moto huo.

“Pamoja na uchunguzi wa awali kuonyesha uwezekano wa moto huo kusababishwa na hitilafu ya umeme, tusibweteke, lazima uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo cha moto huu,” amesema Mtigungwe.

Pia, amesema kama kuna watu wamehusika, wakamatwe na kufikishwa mbele vyombo vya sheria.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Geofrey Mwambe amesema mali mbalimbali za wanafunzi zenye thamani ya zaidi ya Sh25 milioni zimeteketea, huku hasara ya Sh24.3 milioni ikipatikana kutokana na jengo hilo kuharibika.