CAG awasilisha ukaguzi mashirika ya Umoja wa Mataifa

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG), Profesa Mussa Assad

Muktasari:

Ripoti hizo zimepitishwa juzi kwenye kikao cha 71 cha bodi hiyo kinachoendelea jijini New York Marekani kilichohudhuriwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG), Profesa Mussa Assad.

Dar es Salaam. Bodi ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya Umoja wa Mataifa (UNBOA) imepitisha ripoti 28 zikiwamo 11 zilizofanywa nchini.

Ripoti hizo zimepitishwa juzi kwenye kikao cha 71 cha bodi hiyo kinachoendelea jijini New York Marekani kilichohudhuriwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG), Profesa Mussa Assad.

Kikao hicho kinapokea na kuidhinisha ripoti za kaguzi za Umoja wa Mataifa kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2016.

Wakati Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Naot) ikiwasilisha ripoti 11, zilizosalia zilitoka Ujerumani na India.

Profesa Assad na ujumbe wake wamemshukuru Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Modest Mero kwa kurahisisha shughuli za maofisa wa Naot.

“Kwa miaka mitano mfululizo baada ya kujiunga na bodi hii, ofisi imefanikiwa kutoa ripoti kwa wakati,” alisema Profesa Assad.

Ripoti 11 zilizowasilishwa na Tanzania ni ukaguzi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Idadi ya Watu Duniani la Umoja wa Mataifa (UNFPA), Shirika la Ujenzi na Misaada la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi wa Palestina na Mashariki (UNRWA)na Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa UNRWA Wakazi (UNRWA – SPF).

Nyingine ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN– Women), Mfuko wa Ukuzaji Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN Habitat) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP).

Nyingine ni Mahakama ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na Mauaji yaliyotokea Rwanda (ICTR), Mahakama ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na Mauaji yaliyotokea Yugoslavia ya zamani (ICTY) na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kupunguza shughuli za mahakama za kimataifa (IRMCT).

Balozi Mero aliwataka watumishi wa Noat kuendelea kuangalia fursa za ukaguzi katika medani za kimataifa ili kuimarisha na kuendeleza ujuzi na uzoefu uliojengeka kwa muda ambao Tanzania imedumu kwenye bodi hiyo.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri. Mnaipa nchi heshima kubwa hata hivyo niwashauri, ni vyema mkaendelea kutafuta kazi kwenye mashirika mengine ya kimataifa ili kuendeleza ujuzi,” alisema Mero.