Friday, February 17, 2017

CAG mstaafu aonya suala la viwanda

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uwajibikaji

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uwajibikaji Tanzania (Wipa), Ludovick Utouh (katikati) akijadili jambo na washiriki wa warsha ya kukuza uwajibikaji na utawala bora iliyofanyika jijini Dar es salaam jana. Kulia ni Akbar Mohabat na Deogratias Laballa kutoka Shirika la Miradi la Ujerumani la Giz. Picha na Ericky Boniphace 

By Joyce Mmasi, Mwananchi jmmasi@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh ameonya kuwa sera ya viwanda isipoenda sambamba na uwajibikaji kwa viongozi wa mashirika na taasisi zitakazosimamia, historia ya viwanda kufa inaweza kujirudia.

Utouh pia ametetea Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa madai kuwa ni nzuri na inafaa kufuatwa.

Alisema kitendo cha Serikali kuchelewesha malipo kwa wazabuni kunasababisha gharama za tenda kuwa kubwa.

Akizungumza katika warsha ya Kukuza Uwajibikaji na Utawala Bora iliyoandaliwa na Taasisi ya Wajibu, Utouh alisema ni vema Serikali ikaweka mikakati imara ili historia isije kujirudia.

Utouh, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Wajibu inayojishughulisha na masuala ya kukuza uwajibikaji na utawala bora, akizungumza na wakurugenzi watendaji wakuu wa taasisi binafsi na za umma, alisema miongoni mwa sababu zilizochangia kuua viwanda na mashirika ya umma ni ukosefu wa uwajibikaji kwa waliokuwa wasimamizi.

“Tusingependa historia ikajirudia, tukajenga viwanda vikaishia kufa kama awali. Lazima tuweke mikakati imara na kusisitiza dhana ya uwajibikaji kwa viongozi tutakaowapa dhamana,” alisema.

Hata hivyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage aliiambia Mwananchi jana kwa njia ya simu kuwa ipo tofauti ya viwanda katika Serikali ya Awamu ya Kwanza na ile inayohubiriwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Waziri Mwijage alisema mikakati ya Serikali ni kujenga uchumi wa viwanda kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo.

Utouh alisema madhumuni ya warsha hiyo ni kuzungumzia na kuangalia vitu hatarishi katika utawala bora na utekelezaji wa sheria na taratibu zinavyotaka.

Alisema Serikali inahamasisha kukuza uchumi wa Taifa kwa kutumia viwanda ili kukuza uchumi.

“Hili ni wazo zuri, lakini tunapaswa kuangalia mkakati imara utakaoweza kulipeleka Taifa mbele,” alisema Utouh na kuongeza:

“Baba wa Taifa alijenga viwanda vingi, kila sekta ilikuwa na viwanda, lakini tulifanya nini? Haikuchukua muda, vile viwanda vyote vilisambaratika.”

Alisema itakuwa aibu kama ari na nguvu kubwa inayofanywa na Serikali katika kukuza uchumi wa viwanda ikaishia kwa kujirudia mambo yaliyotokea miaka ya nyuma.

Akizungumzia Sheria ya Ununuzi inayolalamikiwa kuwa inachochea wazabuni kuweka viwango vya juu vya gharama za zabuni, Utouh aliitetea kuwa ni nzuri na kwamba, Serikali ndiyo inachangia kuifanya sheria hiyo ionekane mbaya.

Alisema madhara yanayotokana na ucheleweshaji wa malipo kwa taasisi za kampuni zinazopewa zabuni na Serikali, ndiyo yanayofanya manunuzi yanakuwa makubwa kwa wale waombaji wa zabuni ambao huweka bei kubwa kama njia ya kufidia kucheleweshewa malipo yao. “Sheria ya manunuzi ni nzuri na nia yake ni kuwawezesha wanaoomba tenda serikalini wapate kazi bila kutoa rushwa. Lakini kutokana na Serikali kuwacheleweshea malipo, wafanyabiashara huweka gharama za juu kama riba kwa sababu Serikali haina utaratibu wa kuwalipa riba,” alisema Utouh

Mmoja wa washiriki katika warsha hiyo, Profesa Prosper Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, aliishauri Serikali kutazama suala la kushuka kwa thamani ya shilingi na kuja na mikakati ya kuiinua.

“Tunapaswa kuimarisha shilingi yetu kwa kuhakikisha tunauza nje kiasi cha kutosha na kuzuia manunuzi yasiyo ya lazima,” alisema Profesa Ngowi.

-->