CBT yaibua mradi mpya upandaji wa mikorosho

Muktasari:

Unatarajia kupanda miche milioni 30 katika kipindi cha miaka mitatu kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.

Mtwara. Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Dastani Kaijage amesema bodi hiyo kwa kushirikiana na halmashauri mbalimbali nchini, wameibua mradi mpya wa upandaji miche ya mikorosho.

Unatarajia kupanda miche milioni 30 katika kipindi cha miaka mitatu kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.

Kaijage aliyasema hayo mbele ya Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Suleiman Mzee ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi, katika uzinduzi wa kampeni ya upandaji mikorosho mipya kwa msimu 2016/2017, iliyofanyika katika Kijiji cha Dihimba wilayani Mtwara.

Kaijage alisema ili kuhakikisha malengo ya mradi huo pamoja na agizo la Serikali vinatekelezwa kikamilifu, waatalamu wanatakiwa kutoa elimu kwa wakulima ya namna ya upandaji wa mikorosho hiyo.

Mwanzoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa alitoa agizo kuwa kila kijiji kihakikishe kinapanda wastani wa mikorosho 5,000 kwa mwaka ili kuongeza ubora wa zao hilo.

Mzee alizitaka halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha miche ya mikorosho inasambazwa mara moja kwa wakulima.

Alisema aliwaagiza wataalamu kusimamia kazi hiyo ili mvua zinazoendelea kunyesha zisaidie kuistawisha.