CCM Bagara wajihakikishia ushindi

Muktasari:

Polepole kumnadi Tlaghasi kesho Babati 

Babati. Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Babati mkoani Manyara kimejihakikishia ushindi kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani wa Bagara kutokana na wananchi kuwa na imani na chama hicho.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa CCM wilaya hiyo, Fauswali Dauda wakati akizungumza akimnadi mgombea udiwani wa Bagara, Nicodemus Tlaghasi kwenye mkutano wa kampeni.

Dauda alisema hawana tatizo na ushindi kwani wananchi wana imani na chama hicho na watashinda mapema na kuendelea kuwasogezea maendeleo wananchi wa Bagara.

Akiomba kura, Tlaghasi alisema hana wasiwasi wa kushinda nafasi hiyo kwani wananchi wanatambua namna alivyoshirikiana nao wakati akiwa diwani wa kata hiyo kupitia Chadema.

"CCM ni chama dume ndiyo sababu nikaondoka huko Chadema na kuja kwa wajanja, naombeni kura zenu niwatumikie kwa uhakika zaidi," alisema Tlaghasi.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM mkoa wa Manyara, Jacob Siay alisema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Humphrey Polepole atakuwepo mjini Babati kesho JUlai 24, 2018 kufanya kampeni ya kumnadi mgombea huyo.

"Mnakaribishwa kwenye kampeni mtaa wa Nakwa ili mumsikilize ndugu Polepole atakayekuwepo siku ya Jumanne pamoja na viongozi wengine watahudhuria kwenye kampeni kata ya Bagara," alisema Siay.

Uchaguzi huo utafanyika Agosti 12 mara baada ya Tlaghasi kujiuzulu nafasi hiyo kwa kujiondoa Chadema na kujiunga na CCM akidai kuwa anamuunga mkono Rais John Magufuli na mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti.