Tuesday, April 18, 2017

CCM Zanzibar: Hatuna muda wa malumbano na wapinzani

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdallah

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdallah Juma Abdallah maarufu Mabodi 

By Haji Mtumwa,Mwananchi hmtumwa@mwananchi.co.tz

Zanzibar. Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeeleza kuwa hakina muda wa kuanzisha malumbano na vyama pinzani au kikundi cha watu bali jukumu lake ni kushughulikia maendeleo ya Wazanzibari.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdallah Juma Abdallah maarufu Mabodi alisema hayo alipozungumza katika kilele cha ziara yake ya Mkoa wa Kaskazini Unguja iliyomalizika juzi.

Alisema huu si wakati wa kushughulikia hoja dhaifu za wapinzani au kujiweka katika wakati mgumu wa kuwa na wasiwasi ya utekelezaji majukumu yao.

“CCM haina wasiwasi inaendeleza mbio zake za kusimamia na kuwakumbusha viongozi wakuu kutekeleza ahadi zao kwa wananchi kama kawaida,” alisema

Alifafanua kuwa jukumu la viongozi wa CCM ni kushughulikia mipango ya maendeleo na ustawi wa jamii badala ya kujiingiza katika siasa za malumbano kati yao na wapinzani.

“Kila jambo linalofanywa au kutekelezwa na CCM lipo katika nyaraka za kimiongozo na kisheria ambazo ni Katiba ya Chama, Ilani na miongozo ya maadili na uchaguzi, tofauti na vyama vingine vya kisiasa vinavyoongozwa na matakwa binafsi ya watu wachache,” alisema.

Mabodi alisema chama kitaendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zote zilizoahidiwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita bila ya kujali itikadi za kisiasa au kidini.

Alisema maneno ya wapinzani hayana lengo la kuifikisha CCM pale inapopataka zaidi ya kuwagawa.

Akitoa ufafanuzi kuhusu uchaguzi wa chama hicho unaoendelea kwa ngazi ya matawi, aliwaagiza makatibu na manaibu katibu wa chama na jumuiya zingine kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa ili kila mtu mwenye nia ya kugombea apate nafasi hiyo.

“Kama nikibaini kuna mizengwe au makundi ya kutuharibia uchaguzi ngazi yoyote kwanza watu tuliowapa majukumu watawajibika pia nitawashauri wenzangu kufuta uchaguzi,” alisema.

Awali, akimkaribisha Mabodi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Haji Juma Haji alisema chama hicho kimepitia katika vipindi tofauti vya kiutawala hivyo bado kipo imara kutokana na uzoefu wake.

-->