CCM yaibwaga Chadema Mbeya Vijijini

Muktasari:

Mbunge wa jimbo hilo, Oran Njeza amshinda kwa hoja mpinzani wake, Adam Zella (Chadema)

Mbeya. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimegonga mwamba katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, baada ya Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza (CCM) kuthibitishwa kuwa mbunge halali kwa kumshinda kwa hoja mpinzani wake Adam Zella.

Awali, Zella (Chadema) aliyekuwa akigombea jimbo hilo, alifungua kesi akiitaka Mahakama hiyo kutengua ushindi wa Njeza huku akiwasilisha hoja sita akidai ulikuwa na kasoro nyingi.

Hoja zilizowasilishwa na Zella kupitia kwa wakili wake, Ladislaus Lwekaza na kuungwa mkono na mashahidi 16 ni Njeza kutumia maneno ya ubaguzi wa kikabila kuwatangazia wapigakura kuwa Zella amejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho hivyo apigiwe kura za ndiyo kwa kuwa ndiye mgombea pekee aliyebakia.

Hoja nyingine ni kwamba wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi, Njeza alitoa rushwa kwa wapigakura, kuwapo kwa vituo hewa vya kupigia kura, fomu kuwa na namba za siri zinazofanana na kwamba zilisainiwa na msimamizi mmoja kwa fomu zote.

Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na mawakili wa Serikali, Job Mrema na Haroun Matagane waliokuwa wakiwatetea mlalamikiwa wa kwanza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo.

Jaji, Rose Temba alisema mahakama hiyo inatupilia mbali hoja za mlalamikaji baada ya kusikiliza hoja za pande mbili.

Alisema hoja za mlalamikaji za kuishawishi Mahakama hiyo kutengua ushindi wa Njeza zimekosa mashiko kutokana na mashahidi wake kushindwa kuthibitisha ukweli. “Mahakama hii inamtangaza rasmi, Oran Njeza kuwa mbunge halali aliyechaguliwa kwa kura nyingi na wananchi wa Mbeya Vijijini. Na mahakama inamtaka Zella kulipa gharama zote alizotumia Njeza,” alisema.

Jaji Temba alisema upande wowote ambao haujaridhika na uamuzi huo, upo huru kukataa rufaa ndani ya muda unaopaswa kufanyika na siyo vinginevyo.

Nje ya Mahakama

Zella alisema licha ya kuheshimu uamuzi wa Mahakama katika kesi yake, hakubaliani na mfumo mzima uliotumika.

Alisema Jaji alisoma hoja chache huku akiacha hoja za msingi na kudai haki haikutendeka.

“Kuna hoja kubwa ya tofauti ya kura nilizowasilisha ambazo ni dhahiri nilimshinda Njeza, lakini pale Jaji wala hakugusia kabisa, amekimbilia kusoma hoja nyepesi. Kwa sasa najipanga upya na nitakaa na wakili wangu kuona namna nzuri ya kukataa rufaa,” alisema Zella.

Wakili Joyce Kasebwa aliyekuwa akimtetea, Mbunge Njeza, alisema haikuwa kazi rahisi kushinda kesi hiyo licha ya kwamba hoja zilizowasilishwa na mlalamikaji hazikuwa na mashiko.