Polepole aelezea sababu kushindwa Moshi Mjini

Muktasari:

Polepole amesema chama hicho kimekuwa kikijikuta katika wakati mgumu wakati wa uchaguzi

Moshi.Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewataka viongozi wa chama hicho Manispaa ya Moshi, kuacha kutembea na watu mifukoni na kutengeneza kofia za ubaguzi ndani ya chama kwa kuwa hali hiyo imekuwa ikikigharimu chama wakati wa uchaguzi.

Polepole amesema chama hicho kimekuwa kikijikuta katika wakati mgumu wakati wa uchaguzi kutokana na baadhi ya viongozi ndani ya chama kupenda ubinafsi na kuweka mbele uheshimiwa badala ya utumishi.

Ametoa rai hiyo leo Jumamosi wakati akizungumza  kwenye kikao cha ndani cha Halmashauri Kuu ya CCM Manispaa ya Moshi kilichofanyika mjini Moshi katika ukumbi ulioko kwenye ofisi za chama hicho mkoa ambapo amesema sasa ni wakati wa kujiimarisha ili kuweza kushika hatamu kila ngazi.

Amesema kumekuwepo na baadhi ya viongozi ndani ya chama ambao wamekuwa wakitengeneza makundi ya walionacho na wasio nacho wakati wa uchaguzi hali ambayo imekuwa ikikifanya  chama kushindwa kila mwaka wa uchaguzi katika majimbo mbalimbali likiwemo jimbo la Moshi Mjini.

"Kushindwa kwa CCM  katika majimbo mengi Kilimanjaro hasa hili la Moshi Mjini, kulisababishwa na viongozi, kutembea na majina yao mifukoni na kuweka uheshimiwa mbele badala ya utumishi,  hali hii ilijenga makundi, sasa ni lazima  tubadilike," amesema Polepole