CCM yampelekea Lowassa wabunge 16, vigogo 80 Chadema kumlinda Mbowe Hai

Muktasari:

Mbali na CCM kutangaza kuweka kambi ya wabunge 16 Monduli, Chadema nayo imetangaza kambi ya viongozi 80 kwenye kata mbili za Kia na Machame Uroki zilizopo kwenye jimbo la Hai 

Waandishi wetu

Hai/Monduli. Joto la kampeni za uchaguzi mdogo limezidi kupanda hasa baada ya Edward Lowassa kudai hatishwi na wabunge 16 wa CCM kwenda Monduli, huku Chadema wakipeleka viongozi 80 kwenye kata mbili za jimbo la Hai.

Licha ya vyama vingine kusimamisha wagombea kwenye majimbo matatu na kata 21 za Tanzania Bara, vyama vya CCM na Chadema ndivyo vimepandisha joto la uchaguzi kwenye mikoa miwili ya Arusha na Kilimanjaro.

CCM wamepania kulirejesha jimbo la Monduli lenye historia ya kutoa mawaziri wakuu wawili, Edward Sokoine na Edward Lowassa, lakini kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 jimbo hilo lilikwenda Chadema baada ya Lowassa kuhamia chama hicho.

Mbali na CCM kutangaza kuweka kambi ya wabunge 16 Monduli, Chadema nayo imetangaza kambi ya viongozi 80 kwenye kata mbili za Kia na Machame Uroki zilizopo kwenye jimbo la Hai ambalo mbunge wake ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Wakati CCM wakipania kurejesha hadhi ya jimbo la Monduli lenye historia ya kipekee kisiasa na kiserikali, Chadema wao wanataka kulinda hadhi ya jimbo la mwenyekiti wao Mbowe.

Uchaguzi katika kata hizo unafanyika baada ya waliokuwa madiwani wake, Yohana Laizer wa Kia na Robson Kimaro wa kata ya Machame Uroki kwa tiketi ya Chadema, kujiuzulu na kujiunga na CCM.

Lakini, kinachoonekana kuwaumiza Chadema ni kitendo cha CCM kuwateua Laizer na Kimaro kugombea tena udiwani, kwa maana kama watashinda watashusha hadhi ya mwenyekiti wao na historia ya jimbo kuwa ngome ya upinzani.

Chadema ambayo imewasimamisha Albashiri Kombe kugombea kata ya Machame Uroki na Hassan Kibuo, kuwania kata ya Kia kimeona umuhimu wa kulinda hadhi ya jimbo la Hai kwa kupeleka viongozi wake 80 kuhakikisha kata hizo zinabaki Chadema.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Basil Lema, alisema timu hiyo ya viongozi 80, itahusisha wabunge wawili wa chama hicho wa mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Lema, wabunge hao watakaopiga kambi katika jimbo hilo ni mbunge wa Rombo na mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Joseph Selasini na Grace Kiwelu (Viti maalumu).

“Ni kweli hadi sasa hatujaonyesha kashikashi yoyote lakini nataka nikuhakikishie tumejipanga na leo (jana) tunakwenda Hai na kikosi kikubwa cha wapambanaji,” alisema Lema.

Lema alifafanua kuwa mbali na wabunge na madiwani, lakini timu hiyo itahusisha viongozi wa Chadema wa ngazi ya mkoa na wilaya na watasambaa katika vitongoji vya kata hizo.

Hata hivyo, hakuweka wazi iwapo mbunge wa Hai, Mbowe atakuwa mmoja wa vigogo hao, akisema huenda kiongozi huyo akafika katika mikutano ya lala salama.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Kilimanjaro, Jonathan Mabhia, alisema chama chake kinaendelea na mikutano ya ndani na kampeni za nyumba kwa nyumba katika kata hizo.

Mbali na Hai, kwenye jimbo la Monduli mgombea wa CCM Julius Kalanga ambaye awali alikuwa mbunge jimbo hilo kupitia Chadema, chama chake kimetangaza kupeleka wabunge 16 kuhakikisha jimbo hilo linarudi CCM.

Kwa miaka mingi jimbo la Monduli limekuwa chini ya himaya ya CCM, pia ni jimbo pekee nchini lililoweza kutoa mawaziri wakuu wawili, Edward Sokoine na Edward Lowassa ambaye amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 20.

Lowassa ndiye aliyemuachia jimbo hilo Kalanga katika Uchaguzi Mkuu uliopita, wakati huo Lowassa alikuwa mgombea urais wa Chadema.

Kalanga baada ya kuliongoza jimbo kwa zaidi ya miaka miwili tangu achaguliwe Oktoba 25, 2015, ameamua kuitosa Chadema na kurejea CCM ambako ameteuliwa tena kugombea ubunge.

Hivyo, kufuatia hali hiyo, wabunge 16 wa CCM wameweka kambi katika jimbo hilo, hadi kumalizika uchaguzi, ili kuhakikisha mgombea wa CCM anashinda.

Miongoni mwa wabunge wanaoshiriki kumnadi Kalanga ni Joseph Kasheku maarufu Musukuma (Geita Vijijini), Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, Sixtus Mapunda (Mbinga), Edwin Sanda (Kondoa Mjini), Catherine Magige (Viti maalumu), Dk Godwin Mollel (Siha), Jitu Son (Babati Vijijini) na Dk Stephen Kiruswa (Longido).

Mbunge wa jimbo la Ngorongoro, William Ole Nasha ambaye ndiye meneja wa kampeni za CCM, alisema uchaguzi wa Monduli umerudiwa baada ya wananchi kukosea mtihani wa mwaka 2015 na CCM itashinda mtihani huo.

Lowassa atamba

Lowassa akimnadi mgombea wa Chadema, Yonas Laizer alisema hatishwi na idadi ya wabunge wa CCM waliopangwa kuja kupambana naye katika uchaguzi huo na kwamba hata wakienda zaidi ya 100 Kalanga hatopata ushindi.

“Nimesikia wamepanga wabunge 16 kuja kupambana na sisi. Nasema hata waje zaidi ya mia moja tutawanyoosha,” alisema Lowassa huku akishangiliwa.

Lowassa ambaye kwa maelezo yake anadai alimpigania Kalanga hadi akapata ubunge, ameweka kambi Monduli akimpigania Laizer huku akimtaja Kalanga kuwa msaliti.

Alisema, Chadema walimuamini Kalanga na kumsaidia kuwa mbunge mwaka 2015, lakini amewasaliti wananchi. “Kalanga tulimleta hapa mkamchagua ametusaliti sasa muonesheni adhabu msimchague tena,” alisema.

Huu ni uchaguzi mdogo wa tano baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015. Pia, kuna uchaguzi mwingine mdogo wa sita umetangazwa na NEC utafanyika jimbo la Liwale mkoani Lindi Oktoba 13.