CCM yasema inamsubiri Lowassa ulingoni uchaguzi 2020

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa

Muktasari:

  • Mbali na CCM kuzungumzia kauli hiyo, wabunge wawili wa Chadema, Tundu Lissu na Mchungaji Peter Msigwa wamesema ni haki yake kuwa na matamanio na kwamba muda ukifika chama kitafanya uamuzi.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa kusema atagombea tena urais katika uchaguzi ujao, CCM imesema inamsubiri na ina uhakika itamshinda tena.

Mbali na CCM kuzungumzia kauli hiyo, wabunge wawili wa Chadema, Tundu Lissu na Mchungaji Peter Msigwa wamesema ni haki yake kuwa na matamanio na kwamba muda ukifika chama kitafanya uamuzi.

Lowassa aliweka rekodi ya kuwa mgombea wa upinzani aliyepata kura nyingi baada ya kugombea kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vingine vitatu vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Alipata kura milioni 6.07, takriban mara tatu ya kura ambazo wapinzani wamekuwa wakipata katika chaguzinne za awali. Mshindi alikuwa John Magufuli wa CCM aliyepata kura milioni 8.8.

Waziri huyo mkuu wa zamani ametangaza nia ya kusimama tena kugombea urais wakati alipofanya mahojiano na waandishi wa Nation Media Group jijini Nairobi, Kenya ambako alikwenda kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, lakini CCM imesema asitarajie ushindi.

Alipoulizwa kuhusu tamko la Lowassa, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli si tishio na hayuko katika fikra za chama hicho.

“Katika orodha ya vitu muhimu, Lowassa hatumfikirii kabisa na si tishio hata kidogo,” alisema Polepole ambaye katika uchaguzi uliopita aliapa kuzunguka nchi nzima kumpinga Lowassa.

Polepole alisema kwa sasa chama hicho kimejikita kutekeleza Ilani yake inayotokana na ahadi za wananchi, kama kushughulikia changamoto za uadilifu kwa viongozi ndani ya CCM na Serikali.

“Tunatimiza wajibu wetu vizuri tuliotumwa na Watanzania na kazi inaonekana. Nje ya hapo tunasubiri Watanzania watupatie haki yetu katika uchaguzi ujao, na tumeshajipangia kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 70, kwa hiyo hatumfikirii kabisa,” alisema Polepole.

Hata hivyo, jina la Lowassa limekuwa gumzo katika vikao vya chama hicho tawala na alisababisha wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM kuchukuliwa hatua, wenyeviti wanne wa mikoa kuvuliwa uongozi na uanachama na wengine kadhaa kuadhibiwa kwa njia tofauti.

Hiyo ilitokana na baadhi kuendelea kumuunga mkono baada ya kujivua uanachama wa CCM na kujiunga upinzani, akiwa Waziri Mkuu wa kwanza kufanya hivyo tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992.

Kauli ya Lowassa kutaka kugombea tena urais haikupokelewa vibaya na wabunge wa Chadema.

“Haijatolewa kwenye forum ya kichama na sidhani kama inaruhusu au kuzuia chochote kinachostahili kufanywa na vikao vya chama,” alisema Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki alipoulizwa kuhusu kauli hiyo.

Jibu kama hilo lilitolewa na Msigwa, mbunge wa Iringa Mjini, aliyesema ni kawaida kwa kila mwanasiasa kuwa na matamanio.

Akizungumza kwenye mahojiano na gazeti hili jana, Msigwa alisema mwanasiasa makini hakosi matamanio bali kitakachozingatiwa muda ukifika ni kufuata taratibu za chama.

“Nia yake haiwezi kuwazuia wengine kugombea, hata mimi nitagombea ubunge wa Iringa Mjini 2020. Lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya wanachama wengine kutogombea,” alisema.

“Hata wewe (mwandishi) unaruhusiwa kuwa na matamanio ya maisha yako. Kesho unaweza kupanga kuwa mwanasiasa au mkulima. Ni jambo la kawaida kabisa.”

Msigwa, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ya Chadema, haoni kama kauli ya Lowassa itavuruga mchakato wa kupata mgombea wa chama hicho.

“Mtu kama anataka kugombea na akatishwa na kauli ya Lowassa, huyo si mwanasiasa,” alisema.

Mchungaji huyo wa Kanisa la Vineyard alisema Chadema inahitaji wagombea wengi ili kukifanya chama hicho kupata mgombea mzuri.

“Kila mwenye matamanio ajitokeze, huwezi kuzuia matamanio ya watu. Kikubwa ni kufuata utaratibu,” alisema.

Msigwa alisema Uchaguzi Mkuu wa 2020 utakuwa wa aina yake na upinzani utapata ushindi licha ya changamoto za kisiasa wanazopitia.