Friday, July 21, 2017

CCM yasema mbinu zake mpya za kimkakati zinavutia wapinzani

 

By Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz

Moshi. Wakati baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakitangaza kuhamia CCM, katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho amesema mbinu zake mpya za kimkakati kulingana na kasi ya dunia, ndizo zinazosababisha mwenendo huo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na katibu huyo anayehusika na siasa na uhusiano wa kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga wakati akizungumza na wanahabari mjini Moshi.

Kanali Lubinga alisema hata madiwani wa Chadema wa Jimbo la Arumeru walijiuzulu kutokana na kuvutiwa na utendaji wa Rais John Magufuli.

“Hii sasa ni CCM mpya na Tanzania mpya. CCM tulijifanyia tathmini ya miaka 40 na kuona mapungufu na tumeyarekebisha ndani ya CCM na serikalini. Kasi hii inawavutia wengi,” alisema.

“Tumeanzisha mbinu mpya za kimkakati kulingana na hitaji la jamii. Dunia inakwenda spidi na spidi ya dunia inavyokwenda lazima chama tawala kiendane na spidi hiyo na hitaji la jamii,” alisema.

Kanali Lubinga alisema katika historia ya Tanzania, haijawahi kutokea Serikali ikatekeleza ahadi yake na kufanya mambo makubwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na miezi nane.

“Hii ndiyo imewafanya madiwani wale wa Arumeru waone kumbe tulipokuwa siko, wameamua kurudi ili tuijenge nchi wala hakuna ushawishi wowote. Watanzania wanamkubali Magufuli na CCM,” alisema.

Katibu huyo alisema hata juzi walifungua tawi la madereva wa bodaboda mjini Moshi ambao waliwaeleza kuwa huko nyuma walirubuniwa, lakini wamebaini huko walipokuwa siko.

“Kwa hiyo tumekuja hapa Moshi na tutazunguka wilaya zote kuwasihi wanachama wetu wachague viongozi bora watakaoiongoza CCM mpya. Mwaka 2020 mtajionea wenyewe,” alisema Lubinga.

Wakati katibu huyo akisema madiwani hao wamejiuzulu kwa ridhaa yao, Chadema wamedai kuwa walishawishiwa na CCM.

Katibu wa Chadema wa Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alikaririwa akisema wana ushahidi kuwa madiwani walishawishiwa kujiuzulu, ikiwa ni pamoja na kuahidiwa vyeo na kazi, madai ambayo tayari madiwani hao wameyakanusha.

CCM imeshaweka masharti yanayoweka muda ambao mwanachama mpya atatumia kabla ya kuruhusiwa kugombea.

Madiwani waliohama Chadema ni Credo Kifukwe, Anderson Sikawa, Emmanuel Mollel, Greyson Isangya na Josephine Mshiu.

-->