CCM yawachomoa madiwani watatu jimbo la Mbowe

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM,, Humphrey Polepole amesema wataendelea kuchomoa wapinzani mmoja mmoja.

Muktasari:

  • Madiwani wote ni wa jimbo la Hai linaloongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na sasa idadi madiwani walioachia madaraka katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha imefikia 12.

Hai. Wakati madiwani watatu wa Chadema wilayani Hai wakihamia CCM, katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho tawala, Humphrey Polepole amesema wataendelea kuchomoa wapinzani mmoja mmoja.

Madiwani wote ni wa jimbo la Hai linaloongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na sasa idadi madiwani walioachia madaraka katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha imefikia 12.

Waliojizulu ni Goodluck Kimaro wa kata ya Machame Magharibi, Abdallah Kassim wa kata ya Weruweru na Evarist Kimathi wa kata ya Mnadani walijiuzulu na kutangaza kuhamia CCM jana.

Akizungumza mara baada ya madiwani hao kujitambulisha, Polepole alisema CCM itaendelea kuchomoa mpinzani mmoja mmoja mpaka watakapohakikisha kuwa siasa ni ushindani wa hoja na si vinginevyo.

Alipoulizwa idadi ya wapinzani waliohamia CCM mpaka sasa, Polepole alisema: “Tuliowapokea rasmi kabisa ni wachache, lakini waliopokelewa katika ngazi za chini ni wengi sana.

“Lakini, kikubwa orodha ya watu ambao wanaomba kujiunga ni kubwa. Wapo wabunge, madiwani, wenyeviti wa vyama na makatibu wakuu wa vyama hivyo.”

Arusha ni moja ya mikoa ambayo CCM ilipoteza viongozi wengi, hasa madiwani wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wakati Kilimanjaro imekuwa ngome ya Chadema.

Polepole alisema CCM itahakikisha kura alizopata Rais John Magufuli mwaka 2015 zinaongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 75.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya wapinzani kuwa CCM inawanunua viongozi wa Chadema, alihoji kama chama hicho kilimnunua waziri mkuu.

“CCM wametoka watu ambao tulikuwa tunawatafutia namna ya kushughulika nao, wakachomoka kwa spidi. Hii ni dhihaka. Kumnunua waziri mkuu ni kitu kikubwa,” alisema na kuongeza:

“Hizi ndizo siasa chafu, siasa za majitaka. Watu wazima wenye akili zao wanakueleza kuwa yapo matatizo kwenye chama, badala ya kuanza kusema wale wamenunuliwa tazama matatizo yaliyo kwenye chama chako.”

Pia, Polepole aliwataka wana CCM wilayani Hai kuwalinda wanachama hao wapya ili kusiwepo malalamiko ya aina yoyote.

Alisema wana taarifa kuwa wanaohamia CCM kutoka vyama vingine wamekuwa ni wahanga wa matukio kama kuhujumiwa na kuzongwa.

Akizungumzia tukio la madiwani hao kujizulu, katibu wa Chadema wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema kuondoka kwa madiwani hao ni sawa na moto uunguzao jabali ili dhahabu safi ibaki na udongo utoke.

“Kinachotokea hakitutishi, kwa sababu ni lazima upepo mkali uje utenganishe chuya na mchele. Huo ndio msimamo wangu,” alisema.

Akizungumza mara baada ya kukaribishwa CCM, Kimaro alisema amerudi nyumbani.

“Tumekuwa na chama kinachodaiwa kina demokrasia, lakini hakina. Ni mtu mmoja mwenye maamuzi yake,” alisema.

Naye Kassim, aliyekuwa diwani wa Kata ya Weruweru alisema: “Nimefanya siasa za kutafuta maendeleo, nikaona labda Chadema kuna demokrasia, lakini hakuna zaidi ya chama kuwa na maamuzi ya mtu mmoja.”

Kwa upande wake, Kimathi alisema kulikuwa na mpasuko.

“Pamoja na Chadema kupata ushindi mkubwa Kata ya Hai, baada ya uchaguzi kuisha, ulitokea mpasuko mkubwa katika halmashauri kiasi cha kushindwa kufanya chochote cha maana. Kumekuwa na migogoro ya mara kwa mara,” alisema Kimathi aliyeenguliwa umakamu mwenyekiti na ambaye aliwahi kupata kesi ya jinai.