CRDB yaanza mchakato kumpata mkurugenzi mtendaji mpya

Muktasari:

  • Dk Kimei mwaka 2017 alitangaza kuwa atastaafu mwaka 2019

Wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei akitarajia kustaafu Mei 2019, benki hiyo imetangaza mchakato wa kumpata mrithi wake.

Mwishoni mwa mwaka 2017, Dk Kimei alitangaza kustaafu na kuipa benki hiyo miezi 19 ya kumtafuta mkurugenzi mpya atakayeiongoza.

Kuanza mchakato wa kumpata mrithi huyo, bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo leo Machi 19, 2018 imetangaza nafasi hiyo na kuwataka watu wenye sifa kutuma maombi yao mpaka Aprili Mosi, 2018.

Tangazo la benki hiyo linasema atakayekidhi vigezo na kupendekezwa na bodi hiyo kuchukua mikoba ya Dk Kimei, anapaswa kuwa na uzoefu usiopungua miaka 15 ya uongozi hasa kwenye taasisi za fedha.