CTI: Viroba kufilisi wawekezaji

Vibarua wakikusanya pakiti za plastiki za kuwekea pombe kali ‘viroba’. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Ni kutokana na agizo la Serikali la kuzuia vifungashio vya plastiki kwenye paketi za pombe kali maarufu kama viroba

Dar es Salaam. Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), limesema katazo la pombe kali ndani ya vifungashio vya plastiki maarufu ‘viroba’, litawaathiri wawekezaji  wenye viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo.

Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi wa CTI, Hussein Kamote alisema utekelezaji huo unakwenda kinyume na maombi yao waliyoyatoa serikalini ya kupewa muda wa miaka miwili.

Kamote alisema lengo la kuomba muda zaidi, lililenga kufanikisha mchakato wa kuhama teknolojia ya vifungashio vya plastiki na kuingia ya chupa.

Juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alieleza utaratibu utakaotumika kuondoa sokoni matumizi ya pakiti za plastiki za kufungashia pombe hizo huku akipiga marufuku utengenezaji, usambazaji na uingizaji nchini wa mifuko hiyo.