CUF wasema Profesa Lipumba hajaingia mitini

Muktasari:

Ujio wa Profesa Lipumba umeahirishwa zaidi ya mara tatu, na ndiye mara zote alikuwa akitajwa kuwa angezindua kampeni za chama hicho Jimbo la Siha.


Siha. Chama cha Wananchi (CUF), kimesema mwenyekiti wao wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, hajaingia mitini katika kumnadi mgombea wao ubunge Jimbo la Siha, Tumsifuel Mwanri.

Ujio wa Profesa Lipumba umeahirishwa zaidi ya mara tatu, na ndiye mara zote alikuwa akitajwa kuwa angezindua kampeni za chama hicho Jimbo la Siha.

Awali mgombea huyo, amekaririwa akisema chama hicho kingezindua kampeni Januari 27 katika kijiji cha Miti mirefu na mgeni rasmi angekuwa Profesa Lipumba, lakini hata hivyo hakutokea siku hiyo.

Hata hivyo, baada ya kutotokea, chama hicho kikatoa taarifa kuwa Profesa Lipumba angezindua kampeni za chama hicho Februari 8 katika mji wa Sanyajuu ingawa nako hakutokea.

Pamoja na kutotokea, mgombea wake wa ubunge ameendelea na kampeni zake akinadiwa na Naibu Mkurugenzi wa ulinzi na usalama wa CUF Taifa, Masoud Omar hali inayozua minong’ono.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 9, Omar amesema, Profesa Lipumba hajaingia mitini kwenye kampeni za Jimbo la Siha na kwamba kilichotokea ni ratiba zake kuingiliana na za Siha.

Omar amesema kuna baadhi ya watu katika Jimbo hilo wanaeneza uvumi  kuwa Profesa Lipumba amemtelekeza mgombea wao jambo alilosema si kweli bali wanaendelea kufanya mawasiliano naye na atafika jimboni humo.

Amefafanua kuwa awali alitakiwa kuzindua kampeni za chama hicho Kata ya Miti Mirefu lakini ratiba ziliingiliana na kutakiwa kwenda Pemba na juzi alikuwa na mkutano na viongozi wa CUF Kinondoni.

“Tunafanya mawasiliano naye atakuja kwenye kampeni wala msitie hofu ili kuhakikisha jimbo tunalichukua na watu wapuuze maneno kwamba Profesa Lipumba ameingia mitini,” amesema.

Akiwa katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Lawate, mgombea ubunge wa CUF, Mwanri, amesema endapo watamchagua kuwa mbunge wao atahakikisha anaiboresha miundombinu ya soko la Lawate.