CUF waichambua bajeti ya Serikali

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, alipokuwa akichambua bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2018/19. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Wataka Serikali kutenga asilimia 10 ya bajeti kwa ajili ya sekta ya kilimo

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimeishauri Serikali kutenga zaidi ya asilimia 10 ya bajeti yake kwa ajili ya sekta ya kilimo ili kufikia azma ya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 24, 2018 na Julius Mtatiro, mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya chama hicho upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Akichambua bajeti ya Serikali iliyowasilishwa Alhamisi iliyopita bungeni mjini Dodoma, Mtatiro amesema bajeti hiyo haijatoa mikakati ya kuinua sekta jumuishi ambazo zinaajiri watu wengi kama kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara na utalii.

 

Amesema kilimo ambacho kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania kila mwaka kinapangiwa bajeti chini ya asilimia mbili, fedha zinazopitishwa na Bunge hazitolewi zote.

Mtatiro amesema uchumi hauwezi kukua kama Serikali haitaweka mikakati ya kuchochea sekta zinazoajiri watu wengi.

"CUF tulitarajia kwamba bajeti itaweka mipango ya kusimamia sekta jumuifu zenye kuajiri watu wengi, lakini hamna kitu. Hakuna usimamizi kwenye mazao muhimu ya biashara, hata korosho iliyoingiza zaidi ya Sh1 trilioni haijawekewa mikakati ya kuiinua zaidi," amesema Mtatiro.

Amebainisha kwamba mwaka 2017 sekta ya uvuvi haikupangiwa kabisa fedha za maendeleo lakini mwaka huu imetengewa Sh56 bilioni ambazo nazo anasema hazitoshi kuinua sekta hiyo.

"Kila mwaka vijana milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira wakati Serikali na sekta binafsi zikiajiri watu wasiozidi 100,000. Hapa kuna tatizo na bajeti kuu haijaliangazia hili,” amesema.