CUF yatangaza wagombea majimbo matatu

Muktasari:

NEC imetangaza uchaguzi mdogo katika majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini utakaofanyika Januari 13,2018.

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) upande unaomuunga mkono Mwenyekiti wa Taifa anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba umesimamisha wagombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa majimbo matatu.

Uchaguzi uliopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanyika Januari 13,2018 utafanyika katika majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya amewataja wagombea hao na majimbo yao kwenye mabano kuwa ni Delfina Mlelwa (Singida Kaskazini), Japhary Mneke (Songea Mjini) na Kisiongo Mayasek Olukuya (Longido).

Uteuzi huo umefanyika siku chache baada ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutishia kutoshiriki uchaguzi huo endapo NEC haitasitisha mchakato na kujadili dosari zilizojitokeza katika uchaguzi wa awali.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa niaba ya Ukawa, alisema uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 uliofanyika Novemba 26,2017 ulikuwa na dosari zinazopaswa kujadiliwa kabla ya kufanyika uchaguzi mwingine.