CUF yataka mashamba ya wanaCCM nayo yafutiwe umiliki

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi jana, mwenyekiti wa CUF mkoa wa Morogoro, Abeid Mlapakolo alisema kuna vigogo wengi wa CCM wanaomiliki mashamba makubwa mkoani hapa ambao hawayaendelezi.

Morogoro. Chama cha Wananchi (CUF) Morogoro kimeipongeza Serikali kwa hatua ya kufuta umiliki wa shamba la mke wa waziri mkuu mstaafu, Esther Sumaye lakini kimetaka ujasiri huohuo utumike kufuta mashamba mengine yakiwamo ya vigogo wa CCM.

Akizungumza na Mwananchi jana, mwenyekiti wa CUF mkoa wa Morogoro, Abeid Mlapakolo alisema kuna vigogo wengi wa CCM wanaomiliki mashamba makubwa mkoani hapa ambao hawayaendelezi.

“Miaka saba iliyopita wananchi wa Kijiji cha Mvomero lilipokuwepo shamba la Sumaye walinifuata na kuniomba nishughulikie suala hilo maana kijiji kilikuwa kinaongozwa na mwenyekiti kutoka katika chama chetu na nilijaribu kufuatilia bila mafanikio,” alisema.

Lakini kwa kuwa Serikali imeonyesha ujasiri wa hali ya juu wa kumnyang’anya mama Sumaye shamba, mwenyekiti huyo ametaka ujasiri huohuo utumike kurejesha mashamba mengine mengi ambayo hayaendelezwi.

Alisema suala la ukaguzi na uwasilishaji wa orodha ya mashamba pori yanayotakiwa kubatilishwa miliki halifanyiki kwa uwazi na kwamba kuna mengine yanastahili kufutiwa lakini hilo halifanyiki kutokana na majina makubwa ya wamiliki wake.

“Kwa muda mrefu Serikali imetengeneza migogoro katika vijiji vyetu kutokana na kukumbatia watu hawa na kusababisha wananchi kukosa maeneo ya kilimo na pia kuchangia migogoro ya wakulima na wafugaji ya kugombea maeneo madogo yaliyopo kwa kilimo,” alisema.

Mlapakolo alisema watu pekee wenye uwezo wa kumiliki mashamba makubwa bila kuyaendeleza na wasichukuliwe hatua ni wana CCM.

Hata hivyo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Mashariki, Juliana Pilla alisema ubatilishaji wowote wa ardhi unafuata sheria, kanuni na taratibu.

Alisema sheria ipo wazi kwamba ndani ya miaka mitano, mmiliki anatakiwa awe ameendeleza tano ya nane (ambayo ni zaidi ya nusu) ya eneo alilomilikishwa kisheria.

“Niseme tu kwenye majalada ya umiliki wa ardhi niliyonayo hapa hakuna hata moja lililoandikwa kuwa mmiliki huyu ni wa chama fulani, majalada yana majina tu na si vinginevyo,” alisema Pilla.

Alisema kabla haijachukuliwa hatua ya kufuta umiliki wa mashamba pori, huwa wanajiridhisha kwa kufanya ukaguzi na kutoa notisi inayomtaka mmiliki kuendeleza na wanapoona hakuna kinachofanyika ndipo hatua za kubatilisha umiliki zinapofuata.

Alisema sheria pia iko wazi pale mtu anapoona hajatendewa haki akisema kuna hatua za kufuata.

Hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitangaza ubatilishaji umiliki wa ekari 326 zilizokuwa zikimilikiwa na Mama Sumaye lililoko wilayani Mvomero.