CWT yahofia mahitaji Serikali ikihamia Dodoma

Eneo la mji wa Dodoma

Muktasari:

Akizungumza jana, Katibu wa CWT Manispaa ya Dodoma,  Raphael Maswi alisema baadhi ya shule kwa sasa wanafunzi wanasoma kwa kupishana kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Dodoma. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeonyesha hofu juu ya miundombinu ya elimu iliyopo Dodoma iwapo itakidhi mahitaji ya Serikali kuhamia huko kwa mkupuo.

Akizungumza jana, Katibu wa CWT Manispaa ya Dodoma,  Raphael Maswi alisema baadhi ya shule kwa sasa wanafunzi wanasoma kwa kupishana kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

“Miundombinu ya elimu kama madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo bado haitoshelezi mahitaji,” alisema.

Alisema ni vyema Serikali ikahamia kwa awamu katika kipindi cha miaka minne iliyosalia ya awamu ya tano ili kuepusha usumbufu kwa watumishi na familia zao.

“Mimi mwenyewe nilipohamia hapa ingawa nilikuwa peke yangu, nilipata shida ya kupata nyumba ya kuishi, sasa hapo watakapokuja wengi hali itakuwaje?” alihoji.

Hata hivyo, alisema kuhamia kwa Serikali mjini hapa kutawezesha kupata huduma kwa urahisi na kupunguza safari kwa watumishi wa umma.

Alisema kwa kuwa Tume ya Utumishi ya Walimu ina makao makuu yake mjini Dodoma, walimu watakuwa wamepunguziwa usumbufu wa safari na msongamano wa Dar es Salaam.