Chadema, Mwakyembe wavutana

Tundu Lissu

Muktasari:

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani alitangaza kupiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa juzi akisema inalenga kuhamasishana kufanya uhalifu.

Dar es Salaam. Hali ya mvutano baina ya Serikali na wapinzani jana iliendelea baada ya Chadema kusema amri ya Jeshi la Polisi ya kupiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa ni haramu, huku Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe akisema ni halali na kutoitii ni kuvunja sheria za nchi.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani alitangaza kupiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa juzi akisema inalenga kuhamasishana kufanya uhalifu.

Lakini jana, Chadema ambayo imetangaza kuanza mikutano na maandamano nchi nzima chini ya operesheni iliyoiita ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) kuanzia Septemba Mosi, ilisema mikutano hiyo hailengi kuhamasisha vurugu.

Imesisitiza kwamba mikutano na maandamano hayo itafanyika kama ilivyopangwa na watafuata taratibu zote za kisheria, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kama Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma inavyotaka.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema Jeshi la Polisi linatumiwa kisiasa ili kuzuia shughuli za vyama vya siasa kwa kuhusisha mpango wa Ukuta na mauaji ya askari wane yaliyotokea Dar es Salaam usiku wa kuamkia juzi.