Chadema ‘wailima’ barua NEC

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji

Muktasari:

Yataka mchakato urejewe, wahusika wachukuliwe hatua


Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kikilalamikia kile kilichotokea Korogwe Vijijini.

Barua hiyo imeandikwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji jana jioni Augusti 21, 2018 imekwenda kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Korogwe Vijijini, Dk George Nyaronga.

Barua hiyo ya Dk Mashinji kwenda kwa Dk Kihamia aliituma baada ya Dk Nyaronga kumtangaza mgombea wa CCM, Timotheo Mzava kupita bila kupingwa.

Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/TU/05/80, nakala yake imetumwa kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, msimamizi wa uchaguzi Korogwe Vijijini, Dk Nyaronga.

“Rejea mazungumzo yetu ya simu awali leo (jana) saa 6:03 mchana na ukanirudia saa 06:06 kuhusu msimamizi wa uchaguzi Korogwe kutopokea fomu ya mgombea ubunge kupitia Chadema, Amina Ally Saguti ambaye alikuwapo muda wote leo (jana) kuanzia saa 4:00 asubuhi ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Korogwe Vijijini, jambo ambalo uliahidi kulighulikia,” anasema Dk Mashinji.

“Nilikurejea tena saa 09:47 jioni kukujulisha kuwa bado msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Korogwe Vijijini hajapokea fomu za mgombea kupitia Chadema na ukanirejea tena saa 09:55 ukinieleza kuwa unashughulikia.”

Katika barua hiyo, Dk Mashinji anasema: “Katika mazingira hayo, tunaitaka ofisi yako na Tume iingilie kati suala hili kubwa la uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili mchakato urejewe kuruhusu mgombea wetu wa Chadema na wengine waliochukua fomu za uteuzi waweze kurejesha fomu hizo kwa ajili ya uteuzi.”

“Pamoja na kuingilia suala hili, tunaitaka pia ofisi yako iitishe mara  moja kikao cha maadili cha Taifa kwa ajili ya kumjadili msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Korogwe Vijijini na OCD (mkuu wa polisi wilaya) wa Korogwe ili hatua kali za nidhamu zichukuliwe dhidi yao na wote  wanaohusika,” amesema Dk Maashinji